Na Mwandishi Wetu,TimesMajira
Hospitali ya Taifa Muhimbili–Mloganzila imefanya jumla ya upasuaji 500 wa kubadilisha nyonga na goti kwa wagonjwa wenye changamoto za viungo hivyo tangu mwaka 2022 hadi Septemba 2026, hatua inayoonesha kuendelea kuimarika kwa huduma za kibingwa bobezi za mifupa na viungo katika hospitali hiyo.
Kwa mujibu wa takwimu za hospitali hiyo, wagonjwa 500 walifanyiwa upasuaji wa kubadilisha goti na upasuaji wa kubadilisha nyonga huku wengine wakifanyiwa upasuaji wa marudio wa kurekebisha goti lililowahi kufanyiwa upasuaji (revision arthroplasty surgery)
Akizungumza kuhusu huduma hiyo, Daktari Bingwa Mbobezi wa Upasuaji wa Nyonga na Magoti MNH–Mloganzila, Dkt. Shilekirwa Makira, amesema huduma hiyo imeendelea kukua tangu ilipoanza mwaka 2022, ambapo wagonjwa sita walifanyiwa upasuaji huo, idadi iliyoongezeka hadi 104 mwaka 2023 na kufikia 150 mwaka 2024. Mwaka 2025, wagonjwa 91 walifanyiwa upasuaji huo, huku wagonjwa 71 wakiwa wamefanyiwa huduma hiyo hadi Septemba 2026.
Dkt. Makira amesema takribani asilimia 76 ya wagonjwa waliofanyiwa upasuaji huo ni wanawake, huku umri wao ukiwa kati ya miaka 21 na 91. Aidha, zaidi ya robo tatu ya wagonjwa walikuwa na umri wa miaka 60 au zaidi.

Ameeleza kuwa sababu kuu ya wagonjwa kufanyiwa upasuaji huo ni uchakavu wa viungo vya goti na nyonga, unaoweza kuhusishwa na umri mkubwa, uzito mkubwa, majeraha ya viungo, urithi na jinsia ya kike. Magonjwa kama selimundu, jongo na baridi yabisi pia yanaweza kuathiri viungo hivyo.
Kuendelea kutolewa kwa huduma hiyo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili–Mloganzila kunapanua fursa kwa wananchi wenye matatizo makubwa ya goti na nyonga kupata matibabu ya kibingwa bobezi, huku hospitali ikiendelea kuimarisha uwezo wake wa kutoa huduma za kisasa za upasuaji wa mifupa na viungo.

More Stories
Mgejwa:Nishati Safi ya Kupikia ni fursa ya kiuchumi
Tanzania kujenga Chuo Kikuu cha Usafirishaji cha Kanda
TANESCO kuongeza upatikanaji wa Umeme Katavi