October 15, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

GOODWILL yazindua miradi ya upanuzi wa kiwanda Mkuranga

Na Mwandishi Wetu, Mkuranga

Kampuni ya Goodwill (Tanzania) Ceramic imezindua ujenzi wa miradi miwili mikubwa ya upanuzi wa kiwanda chake kilichopo Mkiu, Wilaya ya Mkuranga, Mkoa wa Pwani, ikiwemo Laini ya Tatu ya Uzalishaji wa Vigae na Awamu ya Pili ya Uzalishaji wa Vyombo vya Kaure (udongo) vya Matumizi ya Kila Siku.

Miradi hiyo inatarajiwa kukamilika na kuanza uzalishaji kamili Juni 2027, ikiwa na lengo la kuongeza uwezo wa uzalishaji, ajira na ushindani wa bidhaa za Tanzania katika masoko ya ndani na nje ya nchi.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Stanslaus Haroon Nyongo, amesema Serikali itaendelea kushirikiana na sekta binafsi kutatua changamoto zinazokabili viwanda, huku akiwataka wawekezaji na wafanyakazi kuzingatia nidhamu, uvumilivu na uadilifu katika shughuli zao.

“Serikali tunafanya ziara mara kwa mara kukagua miradi ya sekta binafsi ili kubaini changamoto zinazowakabili na kutafuta ufumbuzi wa mambo ambayo Serikali inaweza kuyatatua. Ndiyo maana hata leo nimeamua kuja hapa pamoja na wenzangu kuona changamoto zilizopo na namna tunavyoweza kuzitatua,” amesema Nyongo.

Amesema kiwanda hicho kina mchango mkubwa katika kutoa ajira kwa wananchi, kikiajiri zaidi ya watu 500 moja kwa moja na zaidi ya 300 kupitia ajira zisizo za moja kwa moja, hivyo kutatua changamoto zake kutasaidia kupanua shughuli zake na kuongeza fursa za ajira.

Nyongo pia amesisitiza umuhimu wa vijana kutumia fursa zinazopatikana katika sekta za viwanda na kilimo kujikwamua kiuchumi, huku akiwataka kuwa wavumilivu na kuepuka vitendo vya udokozi vinavyoweza kuathiri shughuli za uzalishaji na maendeleo ya viwanda.

Amesema Serikali itaendelea kufuatilia changamoto za kiwanda hicho ili kuhakikisha wazalishaji wa ndani wanapata fursa sawa za kushindana katika masoko ya kikanda.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga, Mwinyi Ahmed Mwinyi, Katibu Tawala Wilaya ya Mkuranga Omari Mwanga alisema
Wilaya hiyo ina mpango wa kuanzisha kongani kubwa ya viwanda hatua inayolenga kuongeza ajira, kupanua shughuli za kiuchumi na kuongeza mapato ya Halmashauri.

Amesisitiza kuwa ushirikiano wa wananchi katika kupokea wawekezaji ni muhimu katika kufanikisha ajenda ya maendeleo ya viwanda nchini na kuhakikisha jamii inanufaika na uwekezaji unaofanyika katika maeneo yao.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Goodwill (Tanzania) Ceramic Co., Ltd, Xiaoming Xie, amesema upanuzi huo ni hatua muhimu katika uwekezaji wa kampuni hiyo nchini Tanzania, ukilenga kuongeza uzalishaji na kupanua soko la bidhaa zinazotengenezwa nchini.

“Tunajivunia kuendelea kupanua uwekezaji wetu nchini Tanzania. Nchi hii ina utajiri mkubwa wa madini na msingi mzuri wa uzalishaji wa bidhaa zenye thamani ya juu. Tunaamini upanuzi huu utatusaidia kuongeza uzalishaji, kutengeneza ajira na kupeleka bidhaa zenye alama ya ‘Made in Tanzania’ katika masoko ya Afrika na Ulaya,” amesema Xie.

Amesema miradi hiyo inayotarajiwa kukamilika na kuanza uzalishaji kamili ifikapo Juni 2027, uwezo wa kiwanda unatarajiwa kufikia mita za mraba 180,000 za vigae kwa siku na zaidi ya vipande 200,000 vya bidhaa za kaure kwa siku.

Xie amesema uwekezaji wa jumla wa kampuni hiyo nchini unatarajiwa kufikia dola za Marekani milioni 200, huku upanuzi huo ukitarajiwa kuongeza idadi ya wafanyakazi wa moja kwa moja hadi takribani 4,000, ikijumuisha ajira mpya 1,000, pamoja na fursa takribani 15,000 za ajira zisizo za moja kwa moja.

Ameongeza kuwa zaidi ya asilimia 90 ya malighafi zinazotumika kiwandani hapo zinapatikana nchini Tanzania, zikiwemo udongo na aina mbalimbali za madini, hatua inayochochea shughuli za uchimbaji, uchakataji wa malighafi na kuongeza thamani ya rasilimali za ndani.

Kuhusu changamoto za biashara ya kikanda, Xie amesema kampuni hiyo inakabiliwa na tozo kubwa za ushuru wa bidhaa za vigae vinavyosafirishwa kutoka Tanzania kwenda Kenya, hali ambayo alisema inaweka wazalishaji wa Tanzania katika mazingira yasiyo sawa ya ushindani.

Amesema kampuni hiyo inaiomba Serikali kusaidia kushughulikia suala hilo kupitia Jumuiya ya Afrika Mashariki ili kuweka mazingira ya biashara yenye usawa na kurahisisha upatikanaji wa masoko kwa wazalishaji wa nchi wanachama.