November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wadau wa kemikali wapigwa msasa

Na Daud Magesa, TimesMajira Online, Mwanza

SERIKALI katika kukabiliana na madhara yanayotokana na usimamizi duni wa kemikali imewataka Wasimamizi na Wasafirishaji kuzingatia sheria ya usimamizi na udhibiti kulinda afya za watu na mazingira.

Hayo yameelezwa leo jijini Mwanza na Mkuu wa Wilaya ya Ilemela,Hassan Masala wakati akifungua mafunzo ya siku mbili ya kuwajengea uwezo wasimamizi wa kemikali viwandani na migodini pamoja na madereva wanaosafirisha,Kanda ya Ziwa.

Amesema usimamizi na usafirishaji usio salama wa kemikali hatarishi na zisizo hatarishi unaweza kusababisha madhara,hivyo ni vema wasimamizi na madereva wakazingazitia sheria ya usimamizi na udhibiti wa kemikali katika matumizi na usafirishaji wake ili kuepusha athari kwa watu na mazingira.

“Kemikali tunakutana nazo katika mazingira ya shughuli za kiuchumi hasa viwandani,migodini na kilimo pamoja na bidhaa tunazotumia zinahitaji kemikali kuzitengeneza ingawa zina faida nyingi kwa maisha yetu ya kila siku,”amesema Masala.

Pia udhibiti wa uhifadhi,matumizi na usafirishaji wa kemikali umeiwezesha serikali kutambua aina ya kemikali zinazoingia nchini na zinakopelekwa pia matumizi yake,hivyo sheria ya kusimamia na kudhibiti inalenga kuhakikisha zinatumika kwa usalama bila kuleta athari kwa jamii na mazingira.

“Kupitishwa na kuanza kutekelezwa kwa sheria hiyo,udhibiti wa kemikali umekuwa wa kiwango cha juu tangu kuingizwa, kusafirishwa na matumizi pamoja na mafanikio hayo,jitihada za kuboresha na kuimarisha zaidi usimamizi na udhibiti kupitia maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali mafunzo mbalimbali yanaendelea kutolewa kwa wadau kuhakikisha wananchi wanalindwa dhidi ya madhara yanayotokana na kemikali,”amesema Masala.

Mkuu huyo wa Wilaya ameeleza kuwa kemikali kwa asili zisipotumika kwa usalama unaotakiwa zinaweza kusababisha madhara makubwa kiafya na mazingira licha ya kuwa na faida.

Kwa mujibu wa sheria kila msimamizi wa kemikali,viwandani, migodini na mashambani wakiwemo wasafirishaji na watumiaji wanatakiwa kupata mafunzo maaulum ya matumizi salama ya kemikali na serikali inatambua jukumu hilo na matakwa ya sheria kwa madereva na wasimamizi.

Masala ameeleza zaidi kuwa wasimamizi wa kemikali na madereva wanaozisafirisha ni kundi muhimu na halina budi kupata mafunzo ya uelewa wa madhara ya kemikali,hivyo mafunzo hayo muhimu yatawajengea uwezo na uelewa zaidi.

“Sheria inamtaka kila mwekezaji kuwa na wasimamizi na madereva waliopata mafunzo maalumu ya umahiri wa usimamizi na usafirishaji salama wa kemikali, hivyo naamini mafunzo haya yatawawezesha kupata uelewa na vyeti vya usimamizi na usafirishaji salama wa kemikali ili kulinda afya za watu na mazingira na mtakuwa mabalozi wa kusambaza elimu maeneo mnakofanyia kazi,” amesema Masala.

Naye Meneja wa Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali,Kanda ya Ziwa,Musa Kazumila amesema mafunzo hayo yanalenga wasimamizi wa kemikali viwandani, migodini na madereva wanaosafirisha,kuwapa uelewa namna zinavyosafirishwa na zinavyosimamiwa kwa usahihi ili kulinda afya za watu na mazingira.

“Changamoto za ajali zinazotokana na kemikali zingine ni kukosa uelewa,pia kutosimamiwa ipasavyo migodini kumewasukuma kutoa mafunzo hayo kwa kuwa mamlaka ndiyo msimamizi wa sheria ya udhibiti,inawajibu wa kutoa mafunzo pia ni takwa la kisheria kwamba huwezi kusafirisha kemikali bila kuwa na dereva na msimamizi aliyepitia mafunzo hayo,”amesema.

Kwa upande wake mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo Emmanuel Daniel,ameshauri elimu hiyo isiishie kwa madereva na wasimamizi tu ifikishwe kwenye jamii sababu inaweza kupata madhara inapotokea ajali.

Pia waajiri wawajenge uwezo watumishi wao kwani baadhi ya madereva wanaosafirisha kemikali wako hatarini kupata madhara ya kemikali kwa kulala kwenye magari sababu ya kulipwa maslahi madogo.