May 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wizara ya viwanda, biashara na uwekezaji yawasilisha bajeti ya mwaka 2023/2024

Na Doreen Aloyce, TimesMajira Online,Dodoma

Wizara ya Uwekezaji,Viwanda na Biashara imeliomba Bunge la Jamhuri wa Muungano wa Tanzania kupitisha bajeti ya zaidi ya bilioni 119 (119,017,998,000) ambazo zitaendesha matumizi mbalimbali ya Wizara hiyo.

Ombi hilo limetolewa na Waziri wa Viwanda , Biashara na Uwekezaji Dkt. Ashatu Kijaji wakati akiwasilisha hotuba ya bajeti ya Wizara hiyo Bungeni Dodoma kwa mwaka 2023/2024 ambapo amesema kati ya fedha hizo,zaidi ya bilioni 75.5(75,451,494,000)ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida,huku bilioni bilioni 63(63,086,267,000)ni mishahara na 12,365,227,000 ni matumizi mengineyo.

Amesema bilioni 43.5(43,566,504,000), zinaombwa kwa ajili ya matumizi ya maendeleo ambapo kati ya hizo bilioni 30.3(30,346,819,000) ni fedha za ndani na bilioni 13.2 (13,219,685,000)ni fedha za nje.

Katika kipindi cha Julai, 2022 hadi Machi,2023, mambo mengi yamefanyika ikwemo serikali kupitia Benki ya Maendeleo ya Kilimo ilitoa mikopo ya bilioni 47.042 ili kuwezesha uwekezaji katika viwanda vya uchakataji na uongezaji thamani wa mazao mbalimbali nchini.

“Mikopo iliyotolewa imefanikisha uwekezaji katika viwanda vipya 5 na viwanda 9 vilivyokuwepo kupitia mikopo ya uendeshaji na ununuzi wa mashine za kisasa huku mikopo iliyotolewa kwa viwanda vipya inajumuisha kiwanda kikubwa cha uzalishaji wa sukari kilichopo Bagamoyo ambacho kimeanza uzalishaji kwa kusaga tani 1,500 za miwa kwa siku,”amesema Dkt.Kijaji.

Pia amesema serikali imewekeza katika kiwanda cha kukoboa mpunga na utengenezaji wa chakula cha mifugo chenye uwezo wa kukoboa tani 192 za mpunga kwa siku pamoja na kutengeneza tani 240 za chakula cha mifugo kwa siku.

Dkt. Kijaji amesema kuwa kwa mwaka wa fedha 2023/2024, Wizara imepanga kutekeleza malengo ya kuboresha mazingira ya biashara hapa nchini na nje ya nchi kwa kuanzisha muundo wa ufuatiliaji na tathmini wenye ufanisi katika kukuza biashara.

Vilevile kuhamasisha na kuratibu majadiliano ya kisekta yanayopelekea maboresho ya mazingira ya biashara na kuhakikisha majukumu ya mamlaka za udhibiti yanayoingiliana yanaondolewa na yanayofanana yanaunganishwa.

“Lakini pia malengo ya Wizara katika kuboresha viwanda ni kuwa na takwimu, tathmini na taarifa zitakazowezesha kuendeleza sekta ya viwanda, kuwezesha uanzishwajiwa viwanda vipya na kongani za viwanda,kuendelea na utekelezaji wa miradi ya kimkakati na kielelezo,”amesema Dkt. Kijaji na kuongeza kuwa “Kufanya majadiliano na mwekezaji ili kusaini mkataba wa ubia pamoja na kulipa leseni za uchimbaji wa makaa ya mawe Katewaka,kufanya utafiti wa kina wa kijiolojia na kulipia leseni za uchimbaji katika mradi wa makaa ya mawe Muhukuru,”.

Aidha amesema serikali ina mkakati wa kuendeleza kiwanda cha KMTC katika Mkoa wa Kilimanjaro kuendelea kutafuta masoko kwa ajili ya bidhaa zinazozalishwa hapa nchini ili wananchi waweze kufaidika.