April 30, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wachezaji wampa kigugumizi Sven

Na Mwandishi Wetu

KOCHA mkuu wa mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara (VPL), Simba, Mbelgiji, Sven Vandenbroeck ameendelea kupata wakati mgumu kuweka wazi ni wachezaji gani hasa ambao hawatakuwepo ndani ya kikosi hicho msimu ujao.

Licha ya hadi sasa kukabidhi ripoti ya mapendelezo yake kwa viongozi wa klabu hiyo, lakini bado kocha huyo ameshikilia msimamo wake akidai kuwa bado anapata wakati mgumu kusema ni nani na nani wataondoka ili kupisha nafasi za wachezaji wanaowawania kutoka timu mbalimbali za ndani na nje ya nchi.

Amesema, endapo ni lazima kwake kufanya usajili basi wachezaji anaowahitaji kuboresha kikosi chake ni viungo washambuliaji pamoja na beki ambao watakwenda kuiongezea nguvu safu yake ya ulinzi.

Kinachomlazimu kocha huyo kufanya maboresho hayo ni ushiriki wao katika mashindano ya kimataifa ya Ligi Mabingwa Afrika kwani hadi sasa klabu hiyo ina asilimia kubwa ya kutetea taji lao kwa msimu wa tatu mfululizo kutokana na kudumu kileleni mwa msimamo wa Ligi kwa muda mrefu wakiwa na pointi 71 wakiwazidi Azam wanaoshika nafasi ya pili pointi 17 huku wakiwazidi Yanga pointi 20.

Katika mashindano hayo, Simba wanataka kuhakikisha wanafanya vema na kufika hata nusu fainali au fainali, hivyo ni lazima waboreshe kikosi chao kwa kuongeza wachezaji wenye hadhi ya kupambana na timu bora hasa zile za Waarabu ambao mara nyingi wamekuwa wakiwapa shida.

Kocha huyo alisema kuwa, katika usajili wake atahakikisha anachukua wachezaji bora zaidi watakaoweza kunasa haraka mbinu zake kwani atahakikisha wanacheza zaidi kwa kutumia mfumo wa kusukuma mbele mashambulizi ambao umewafa mafanikio makubwa makocha wa Uingereza Pep Guardiola na Jose Mourinho.

Lakini licha ya kugusia usajili wake, kocha huyo ameweka wazi kuwa, haoni sababu ya kufanya usajili wa washambuliaji ndani ya kikosi chake wakati wale waliopo wanaweza kumpa kile anachokihitaji.

Amesema kuwa, nafasi hiyo ambayo kwa sasa inaundwa na Meddie Kagere, Nahodha John Bocco na Miraji Athumai itasalia kama ilivyo kwani baada ya kukaa nje kwa muda mrefu Miraji ameshaanza mazoezi mepesi na anaamini kuwa hadi mwisho wa msimu mchezaji huyo atakuwa fiti alimilia 100 na kurudi kwenye ushindani kwani kama aliweza kufunga goli sita kwa mechi alizocheza, basi anauwezo wa kufanya makubwa zaidi.

Akijibu maswali aliyoulizwa na mashabiki wa klabu hiyo, kocha huyo amesema kuwa, kwa sasa kitu kinachomuumiza kichwa ni kuhakikisha anasuka kikosi bora kitakachoweza kulipa kisasi kwa wapinzani wao Yanga ambao waliwafunga goli 1-0 katika mchezo wa marudiano wa Ligi Kuu.

Amesema, kilichowafanya kupoteza mchezo huo ilikuwa ni dharau waliyoonesha kw timu hiyo kwani kutokana na kuwaacha nyuma kwa pointi nyingi kwenye msimamo wa Ligi kuliwafanya waamini kuwa mchezo ungekuwa mwepesi na wao kupata ushindi.

Mbali na Yanga kuwapa wakati mgumu lakini pia kocha huyo amezitaja timu za JKT Tanzania ambao waliwafunga na Lipuli ambao licha ya kuwafuga lakini waliwapa wakati mgumu sana.

Kupoteza mchezo dhidi ya JKT, kulikomfanya kocha huyo kubadili mfumo wake wa matumizi ya mshambuliaji mmoja na kutumia washambuliaji wawili jambo ambalo lilimpa matokeo chanya huku akiweka wazi kuwa sababu kubwa za kumtumia Kagere pekee ilikuwa ni majeraha yaliyokuwa yakiwakabili Bocco na Miraji.

Wakati huohuo, zikiwa zimepita wiki kadhaa baada ya kuenea kwa taarifa kuwa miamba ya soka hapa nchini, Simba na Yanga zimeingia vitani kuwania saini ya kiungo wa Namungo FC, Lucas Kikoti, sasa ni rasmi vita hiyo imeibuka upya baada ya kumtaja mchezaji huyo.

Timu hizo zote zimetajwa kumuwinda kiungo huyo ambaye hadi sasa ameshapachika wavuni goli nne huku akifanikiwa kutoa pasi za mwisho za magoli sita ili kuimarisha vikosi vyao.

Kwa mara ya kwanza timu hizo zilipohusishwa kumuwania kiungo huyo, uongozi wa Namungo FC iliwataka vigogo wa timu hizo kukaa meza moja na viongozi ili kuzungumza jambo hilo na si kutumia njia za panya za kufanya nae mazungumzo kwani wao kama viongozi hawawezi kumzuia.

Hata hivyo maneno ya viongozi hao yalitofautiana na yale ya kocha wao,Thiery Hitimana ambaye ameuomba uongozi wa timu hiyo kuhakikisha kiungo huyo tegemeo anabaki ili waendelee kuwa na timu yenye ushindani msimu ujao.

Kocha Sven ameweka wazi kuwa, anavutiwa sana na kiwango cha mchezaji huyo ambaye amekuwa akimfuatilia katika mechi zao nyingi za Ligi Kuu kabla ya Serikali kutangaza kusimamisha shughuli za michezo kwa siku 30 kutokana na virusi vya ugonjwa wa Corona (Covid-19).

Kocha huyo amesema, hata katika mchezo wao dhidi ya Namungo uliochezwa Januari 29, katika uwanja wa Taifa mchezaji huyo alifunga goli zuri baada ya kupiga shuti kali nje ya eneo ya 19.

Katika mchezo huo ambao ulimalizika kwa Simba kupata ushindi wa goli 3-2, Kikosi alifunga goli la pili dakika ya 72 akiisawazishia timu yake ambayo ilikuwa nyuma kwa goli 2-1 na matokeo kuwa goli 2-2 kabla ya mshambuliaji Meddie Kagere kufunga goli la ushindi dakika ya 88.

Goli hilo ndilo lililomfanya kocha huyo kudizi kumfuatilia Kikoti katika kila mchezo waliocheza hadi pale Ligi iliposimamishwa kupisha janga la Corona.

“Miongoni mwa wachezaji wa timu nyingine ninaowakubali ni namaba tisa wa Namungo FC, Lucas Kikoti ambaye alifunga goli zuri katika mchezo wetu ambalo lilinifanya nianze kumfuatilia kwa karibu zaidi, hivyo kwangu naweza kusema yeye ni mchezaji bora sana, ” amesema kocha huyo.

Kitendo cha kocha huyo kumtaja Kikoti kimewakosha mashabiki wa klabu hiyo ambao wamesema kama kocha huyo alikuwa akimfuatili katika mechi kadhaa basi ni wazi jina lake lilishatua mezani kwa vigogo wa klabu hiyo na wameshaanza kulishughulikia hivyo wanachosubiri ni kiungo huyo kutua Simba.