Na Mwandishi Wetu
WAAJIRIWA wapya katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), wametakiwa kuwajibika na kuchapa kazi kwa bidii ili kuendeleza juhudi za kuokoa maisha ya watu wanaokabiliwa na magonjwa ya moyo wanaofika kupata matibabu katika taasisi hiyo.
Rai hiyo imetolewa mapema jana na Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Profesa Mohamed Janabi alipokuwa akizungumza na waajiriwa wapya saba walioajiriwa na Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na kupangiwa kutoa huduma katika Taasisi hiyo.
“Taasisi hii imepata mafanikio makubwa tangu ilipoanzishwa hadi sasa, baadhi yenu mmekuwa sehemu ya juhudi hizi, kwa sababu kwa nyakati mbalimbali mmewahi kujitolea kufanya mafunzo kwa vitendo hapa”.
“Kwa juhudi zile zile endeleeni kuchapa kazi, kila mmoja awajibike katika nafasi yake, mtaona faida ya kazi na juhudi zenu, hakikisheni mnawahi kazini, binafsi huwa sitaki kusikia habari za foleni, mvua kwamba ni sehemu ya sababu ya kuchelewa kufika kazini,” amesisitiza.
Aliongeza “Tuna mafanikio makubwa, tangu kuanzishwa kwa Taasisi hii, miaka minne ya utendaji kazi wetu vifo vilivyotokea katika chumba cha upasuaji mdogo wa bila kufungua kifua kupitia tundu dogo kwenye paja ni asilimia 1.5 yaani sawa na wagonjwa wanane tu waliopoteza maisha katika kipindi chote hicho.
“Tumeweza kupandikiza vifaa visaidizi vinavyousaidia moyo kufanya kazi vizuri (Pacemaker) kwa wagonjwa 56, CRTD kwa wagonjwa wagonjwa 11, tumevuna na kupandikiza mishipa ya damu kwenye moyo (Coronary Artery Bypass Graft – CABG) wagonjwa 82 na tumezibua valvu zilizokuwa zimeziba bila kufanya upasuaji wa kufungua kifua kwa zaidi ya wagonjwa 1,000 hadi sasa,” amesema.
Aliwataka waajiriwa hao kutosita kuuliza wale waliowatangulia kazini mahala popote watakapokutana na changamoto mbalimbali ili kuweza kuzitatua na kuzingatia uvaaji nadhifu wa mavazi yenye staha.
Akizungumza kwa niaba ya waajiriwa wenzake wapya, Daktari Winnie Masakuya amesema wapo tayari kufanya kazi kwa juhudi na maarifa waliyojaliwa na Mwenyezi Mungu katika kuwahudumia wagonjwa wanaotibiwa katika Taasisi hiyo.
“Hatutaiangusha Taasisi yetu,” amemhakikishia Prof, Janabi katika kikao hicho ambacho pia kilihudhuriwa na Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Fedha wa JKCI, Agnes Kuhenga” amesema
More Stories
Amos Lengael Nnko afariki kwa ajali ya gari
Gridi za Tanzania, Kenya kuimarisha upatikanaji wa umeme
Mama Zainab:Watoto yatima ni jukumu la jamii yote