May 15, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Mohamed Ali Shein, Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi-Bara Mzee Philip Mangula na Katibu Mkuu wa CCM Dkt. Bashiru Ally Kakurwa wakiwa katika kikao cha ndani katika Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma. Picha na Ikulu

Magufuli, Dkt. Shein, Mangula, Dkt. Bashiru wateta Chamwino

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

MWENYEKITI wa CCM, Rais John Magufuli amekutana na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, Dkt. Ali Mohamed Shein katika kikao cha ndani kilichofanyika Ikulu, Chamwino Mkoani Dodoma na kuzungumzia masuala mbalimbali kuhusu CCM.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza jambo na Rais wa Zanzibar ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Mohamed Ali Shein Ikulu ya Chamwino Dodoma. Picha na Ikulu

Kikao hicho ambacho kilifanyika jana kilihudhuriwa na Makamu Mwenyekiti CCM Bara, Philip Mangula na Katibu Mkuu wa CCM, Bashiru Ally.

Baada ya kikao hicho, Rais Shein alikwenda kuweka udongo katika jiwe la msingi la ujenzi wa Ofisi za Ikulu na kukagua maendeleo ya kazi ya ujenzi wa ofisi hizo inayofanywa na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kupitia shirika lake la Suma JKT.

Rais Shein alimshukuru, Rais Magufuli kwa kumpa fursa ya kwenda kuweka udongo ikiwa ni kumbukumbu ya ujenzi wa ofisi hizo na amebainisha kuwa kujengwa kwa ofisi hiyo ni heshima kwa Taifa na tafsiri sahihi ya kujitawala.

“Huko ndio kujitawala, kutawaliwa sio kuzuri, mtawala anafanya anavyotaka yeye, anafanya kwa utashi wake pale anapotaka yeye kufanya, tunapochukua hatua ya kujitawala wenyewe tunafanya mambo makubwa kama haya kwa ajili ya wananchi, hii ofisi ni ya wananchi wa Tanzania,” amesema Rais Shein.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza jambo na Rais wa Zanzibar ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Mohamed Ali Shein Ikulu ya Chamwino Dodoma. Picha na Ikulu

Rais Shein aliwasalimu vijana wa JKT wanaofanya kazi za ujenzi wa ofisi hizo, amewapongeza kwa kazi nzuri wanayoifanya na amewataka kujivunia fursa hiyo adhimu ya kujenga ofisi ya Ikulu za nchi yao, badala ya kazi hiyo kufanywa na kampuni za nje ya nchi kama ambavyo hufanyika katika maeneo mengi.