May 15, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mahakama Kuu yatupa kesi dhidi ya Spika, Mwambe

Na Mwandishi Wetu

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam imetupilia mbali kesi ya kikatiba iliyofunguliwa na Wakili, Paul Kaunda dhidi ya Spika wa Bunge, Job Ndugai, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (aG) na aliyekuwa Mbunge wa Ndada, Cecil Mwambe.

Uamuzi huo ulitolewa na mahakama hiyo jana ambapo katika kesi hiyo, Wakili Kaunda alikuwa anaiomba Mahakama Kuu kutengua amri ya Spika Ndugai ya kumtambua Mwambe kama Mbunge halali wa Jimbo la Ndanda, wakati alijiuzulu uanachama wa chama kilichompa ridhaa kwa hiari yake.

Katika uamuzi wake Mahakama Kuu imesema mpeleka maombi (Wakili Kaunda) alikosea kufungu kesi hiyo kwa kutumia kifungo cha kikatiba badala yake alitakiwa kufungua kesi ya kawaida.

Katika uamuzi mdogo uliosomwa jana na Jaji Issa Maige, aliyekuwa akisaidiana na Jaji Stephen Magoiga na Jaji Seif Kulita amesema mlalamikaji alikosea namna ya kufungua kesi ya kikatiba badala yake alipaswa kufungua kesi kwa utaratibu wa kawaida.

Amesema kauli ya Spika Ndugai aliyoitoa haikuwa imevunja katiba, bali ni ya kiutaratibu katika shughuli zake za kiutendaji hivyo mlalamikaji angekuwa sahihi kama angefungua kesi hiyo kwa utaratibu wa kawaida kwa kutumia Ibara ya 83 (1) badala ya ile ya 26 (2) aliyoitumia.

Jaji Maige amesema Ibara hiyo inaenda sambamba na kifungu cha 37 cha Sheria ya Uchaguzi ambacho kinaeleza kuhusu utaratibu wa kutangaza kiti cha Mbunge ambacho kiko wazi.

Wakili Kaunda amefungua kesi mahakamani hapo dhidi ya Ndugai, aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Ndanda kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema)  Cecil  Mwambe  na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Katika kesi hiyo Wakili Kaunda alidai Mwambe alitangaza kujivua uanachama wa CHADEMA na kujiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kauli ambayo iliungwa mkono na Katibu Mkuu wa CCM, Dkt.  Bashiru Ally  aliyempokea rasmi  Mwambe mbele ya hadhira kwa kumkabidhi kadi ya CCM,huku Mwambe naye alimkabidhi Katibu Mkuu huyo  kadi yake ya CHADEMA.

Wakili Kaunda alidai kitendo cha Spika kumtambua  Mwambe kama mbunge halali wakati  ameshajivua uanachama wa chama kilichomdhamini kama Mbunge wa Ndanda ni ukiukwaji wa ibara ya 71(1)(f) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977 na hakuna mamlaka yoyote nchini, achilia mbali Spika, yenye uwezo wa ku mrudisha bungeni Mbunge ambaye kwa hiari yake mwenyewe ameamua kujivua uanachama wa chama cha siasa kilichomdhamini kupata ubunge.