June 13, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Vyuo vitano kunufaika na mradi wa UTT

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

WANAFUNZI wa vyuo vikuu vitano mkoani Mbeya wanatarajiwa kushiriki katika mradi wa University Tourism Tour (UTT), unaolenga kuhamasisha ubunifu wa kutangaza vivutio vya utalii kupitia makala, picha, video na teknolojia za kidijitali.

Katibu wa Taasisi ya Ubunifu wa Miradi (TICON), Livvent Japhet, amesema kuwa programu hiyo inalenga kuwajengea vijana uwezo wa kuitangaza Tanzania kwa kutumia ubunifu katika kusimulia historia, utamaduni na vivutio vya utalii.

Amesema TICON imefanya zoezi la kutambua na kurekodi vivutio vya utalii katika mkoa wa Mbeya na kubaini zaidi ya vivutio 300, huku shughuli hiyo ikiendelea katika maeneo mengine ya nchi.

Kwa mujibu wa Japhet, baadhi ya vivutio vya kihistoria na kiutamaduni vya Mbeya havijatangazwa kwa kiwango kikubwa, hali inayotoa fursa kwa wanafunzi kushiriki katika kuandaa maudhui yatakayosaidia kuviongezea mwonekano kwa umma.

Ameongeza kuwa wanafunzi watakaoshiriki mashindano hayo watapatiwa fedha za kuwezesha usafiri na baadhi ya vifaa vitakavyotumika katika kuandaa maudhui ya kutangaza vivutio hivyo.

Vyuo vitakavyoshiriki katika awamu ya kwanza ni Mbeya University of Science and Technology (MUST), Mzumbe University, Catholic University of Mbeya (CUoM), Tanzania Institute of Accountancy (TIA) na Teofilo Kisanji University (TEKU), ambapo washiriki wataandaa makala, picha na video kuhusu utalii, utamaduni, historia na fursa za uwekezaji.

Mkurugenzi wa TICON, Aman George, amesema mradi huo unalenga kuwapa vijana nafasi ya kutumia sauti na mitazamo yao kutangaza rasilimali za utalii zilizopo nchini, huku ukichochea matumizi ya ubunifu na teknolojia za kisasa.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Jiji la Mbeya, Annamary Joseph, amesema elimu ya utalii ikianza kutolewa mapema shuleni inaweza kusaidia kuongeza uelewa wa watoto na vijana kuhusu sekta hiyo, wakati Mkoa wa Mbeya ukiendelea kuwa na vivutio na fursa mbalimbali zinazohitaji kutangazwa zaidi.