May 21, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Vyombo vya habari vyatakiwa kuripoti bila upendeleo uchaguzi serikali za mitaa

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma

KUELEKEA uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka huu wamiliki wa vyombo vya habari na waandishi wa habari nchini wametakiwa kutoa elimu kwa jamii kuhusu uchaguzi bila upendeleo na kuripoti matokeo sahihi ilikufanya uchanguzi uwe wa amani.

Hayo yameelezwa jijini hapa leo,February 13,2024 na Naibu waziri wa Wizara ya Habari,Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Kwa niaba ya Waziri wa Habari,Mhandisi Mathew Kundo wakati akifungua Mkutano wa Mwaka wa Vyombo vya Utangazaji Nchini ulioenda sambamba na kilele cha maadhimisho ya siku ya Utangazaji Duniani,ulioandaliwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA)

Kundo ameeleza kuwa vyombo vya habari vinanafasi kubwa katika kipindi cha uchanguzi hivyo ni vyema kuzielewa kanuni watakazozijadili katika mkutano huo ilikuwa na uelewa wa pamoja wa namna bora ya kufikisha ujumbe kwa jamii.

“Katika kuelekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa Vyombo vya Habari vinatakiwa kuwa mstari wa mbele katika kuzingatia Maadili na kanuni za utoaji Habari kwa jamii kwa maslahi ya Taifa kwani vina wajibu mkubwa katika Taifa letu hivyo ni muhimu kila mmoja kuzingatia taaluma na kutimiza majukumu yake kwa weledi mkubwa,”amesema Mhandisi Kundo.

Aidha Kundo amevitaka vyombo vya habari kuanzisha vipindi vinavyo hamasisha mila na Destiri ya mtanzani ilikuwaelimisha vijana kuhusu tamaduni zao.

“Ni muhimu sana kwenu TCRA kuliangalia suala hili kwa umakini mkubwa kwani Mkifanya hivi itawasaidia sana kufanya kazi kwa ufanisi,na Sisi kama Serikali tunawaahidi kuendeleza ushirikiano uliopo ili kuleta maendeleo kwa jamii, “amesisitiza.

Kwa upande Wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania( TCRA )Jones Kilimbe amewataka watangazaji na waandishi wa habari kuzingatia Madili na kanuni ya kazi zao.

Vilevile amezungumzia suala la uchaguzi ujao wa Serikali za mitaa kuwa,vyombo vya habari vina jukumu la kutoa elimu kwa wapiga kura ikiwa ni pamoja na kuhabarisha umma kuhusu mwenendo mzima wa kampeni bila upendeleo na kutoa ripoti sahihi za siku ya kupiga kura.

Amesema TCRA kama wadau wa Utangazaji watahakikisha wanakuwa bega kwa bega na vyombo vya Utangazaji kwa kuhakikisha wanatoa mwelekeo wa maudhui yenye ubora bila upotoshaji.

“Maudhui ya Utangazaji ni chakula kwa jamii, yanaweza kujenga au kubomoa, kuharakisha maendeleo au kukwamisha hivyo ni jukumu la vyombo vya Utangazaji kujikita katika kuhabarisha umma maeneo yenye tija na kuachana na uchochezi au uvunjifu wa Madili,”amesema

Naye Mwenyekiti wa wamiliki wa Vyombo vya Habari Nchini( MOAT)Samwel Nyala amesema pamoja na kukuza tasnia ya habari bado kuna changamoto mbalimbali ikiwemo gharama kubwa ya leseni hali inayowakwambisha na kuwapa hasara ya uendeshaji .

Kutokana na hali hiyo ameiomba Serikali kuangalia suala hilo ikiwa ni pamoja na kuangalia suala la ruzuku kwa Vyombo vya Habari kutokana na kuwepo kwa mdororo wa Uchumi.

Kwa upande wake mdau wa habari kutoka Chama cha watangazaji (NIBA) Amos Ngosha ameeleza masikitiko yake kuhusu hali ya uchumi wa vyombo vya habari kuwa imedorora kutokana na kukosa ruzuku kutoka Serikalini.

Hivyo ameiomba Serikali kuanzia kutoa ruzuku kwa vyombo vya habari ili viweze kujiendesha.

“Tunashindwa kujiendesha kwa kukosa matangazo, matangazo yetu yamekuwa ni ya waganga wa tiba asili na viongozi wa dini,tunatozwa Kodi kubwa kuliko faida tunayoipata, tunaomba taaluma hii iheshimiwe kwa kutupunguzia gharama za uendeshaji tuache kuwategema watu wa tiba mbadala katika uchumi,”amesema Ngosha.