Na.Mwandishi wetu,Timesmajira
Vyama vya ushirika nchini vimetakiwa kuandaa na kuwasilisha kwa wakati taarifa zao za fedha za mwaka 2025/2026 ili kuwezesha zoezi la ukaguzi wa kisheria litakaloanza rasmi Julai 20 mwaka huu.
Wito huo ulitolewa jana na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Ukaguzi na Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (COASCO), CPA Jeremiah Mugeta, wakati akizungumza katika banda la COASCO lililopo ndani ya banda kuu la Wizara ya Kilimo kwenye Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba).
“Wito wangu kwa wanaushirika ni kuhakikisha wanaandaa taarifa za fedha za mwaka 2025/2026 na kuziwasilisha katika ofisi zetu za mikoa ili mpango wa ukaguzi uliopangwa uweze kutekelezwa kwa wakati. Pia wazingatie sheria na kanuni za uandaaji wa taarifa za fedha ili kupunguza hati zenye dosari,” amesema Mugeta.
Amesema COASCO, kwa kushirikiana na Tume ya Maendeleo ya Ushirika, imejipanga kuhakikisha vyama vyote vya ushirika nchini vinakaguliwa katika mwaka wa fedha 2026/2027 ili kuongeza uwazi, uwajibikaji na kuimarisha utendaji wa vyama hivyo.
Mugeta amesema wananchi waliotembelea banda la Wizara ya Kilimo wamepata elimu kuhusu huduma zinazotolewa na taasisi zilizo chini ya wizara hiyo pamoja na fursa zilizopo katika sekta ya kilimo na ushirika.
“Nimejionea kazi kubwa inayofanywa na Wizara ya Kilimo kupitia taasisi zake. Kuna fursa nyingi katika sekta ya kilimo na ushirika, na wananchi wanaotembelea mabanda haya wanapata elimu na huduma muhimu zinazowasaidia kuongeza tija katika shughuli zao.”
Amesema sekta ya kilimo inaendelea kuwa mhimili wa uchumi wa Tanzania kwa kuchangia zaidi ya asilimia 26 ya Pato la Taifa, huku mazao yanayouzwa kupitia vyama vya ushirika yakichangia zaidi ya dola bilioni mbili kwa mwaka.
“Kilimo kina mchango mkubwa katika maendeleo ya uchumi wa Tanzania. Ushirika nao umeendelea kuwa chachu ya maendeleo kupitia mauzo ya mazao ya wakulima.”
Aidha, amesema COASCO itaendelea kutekeleza jukumu lake la ukaguzi na usimamizi wa vyama vya ushirika ili kuhakikisha vinaendeshwa kwa kuzingatia sheria, kanuni na misingi ya utawala bora.
“Lengo letu ni kuhakikisha wanaushirika wanapata elimu sahihi na vyama vinaendeshwa kwa uwazi na uwajibikaji. Kila mwaka tunatoa ripoti ya ukaguzi inayoonesha hali halisi ya utendaji wa vyama vya ushirika nchini.”
Mugeta amesema hali ya usimamizi wa vyama vya ushirika imeendelea kuimarika, akibainisha kuwa zaidi ya asilimia 16 ya vyama sasa vinapata hati safi za ukaguzi ikilinganishwa na asilimia nne ya miaka iliyopita, huku idadi ya vyama vinavyopata hati zenye dosari ikipungua kutoka takribani asilimia 17 hadi asilimia tano.
Pia ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na Waziri wa Kilimo kwa kuendelea kuimarisha sekta ya ushirika kupitia uwezeshaji wa taasisi zinazosimamia sekta hiyo.
“Tunamshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuimarisha sekta ya ushirika. Sisi COASCO tutaendelea kutekeleza majukumu yetu kwa uadilifu na weledi ili kuhakikisha ushirika unachangia zaidi katika maendeleo ya uchumi wa nchi.”

More Stories
Serikali yaahidi kuimarisha mapambano dhidi ya UKIMWI
TARI Selian yawaalika wakulima maonesho ya Kilimo-biashara
BRELA yawapa elimu ya Urasimishaji Biashara vijana wanaoshiriki Sabasaba