Na Joyce Kasiki, Dar es Salaam
WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga, ametembelea baadhi ya mabanda ya washiriki katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba), ambapo amejionea bidhaa, huduma na ubunifu mbalimbali unaowasilishwa na taasisi za umma, sekta binafsi pamoja na wazalishaji wa ndani.
Katika ziara hiyo leo Julai 8,2026, amesisitiza umuhimu wa kuendelea kuimarisha viwanda vya ndani, kuongeza thamani ya bidhaa na kupanua masoko ya bidhaa za Tanzania ndani na nje ya nchi.
Akiwa katika mabanda hayo Waziri Kapinga alipata fursa ya kusikiliza maelezo kutoka kwa waoneshaji kuhusu shughuli wanazozifanya, mafanikio waliyoyapata kupitia maonesho hayo pamoja na changamoto zinazowakabili katika uzalishaji na biashara.
Aidha, aliwahimiza kutumia maonesho hayo kama jukwaa la kutangaza bidhaa na huduma zao, kujenga ushirikiano wa kibiashara na kuvutia wawekezaji.
Kapinga alisema Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wafanyabiashara na wawekezaji kupitia sera na mikakati mbalimbali inayolenga kukuza sekta ya viwanda na biashara, sambamba na kuongeza ushindani wa bidhaa zinazozalishwa nchini katika soko la kimataifa.
Kwa upande wao, baadhi ya washiriki wa maonesho walieleza kuwa ujio wa Waziri katika mabanda yao umeongeza hamasa na kuwapa fursa ya kueleza mafanikio pamoja na changamoto zinazohitaji utatuzi ili kuongeza uzalishaji na ushindani wa bidhaa za Tanzania.
Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam yamewakutanisha washiriki kutoka Tanzania na mataifa mbalimbali, yakilenga kuhamasisha biashara, uwekezaji, ubunifu na maendeleo ya sekta ya viwanda kupitia maonesho ya bidhaa na huduma mbalimbali.

More Stories
Serikali yaahidi kuimarisha mapambano dhidi ya UKIMWI
TARI Selian yawaalika wakulima maonesho ya Kilimo-biashara
BRELA yawapa elimu ya Urasimishaji Biashara vijana wanaoshiriki Sabasaba