March 28, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Viongozi CCM, wafanyabiashara Arusha washikiliwa tuhuma za rushwa

Na David John Timesmajira Online

WATU tisa wakiwemo Viongozi wa Jumuiya ya Wazazi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Arusha wanashikiliwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoani humo kwa tuhuma mbalimbali za rushwa.

Taarifa iliyotolewa na Takukuru Mkoa wa Arusha, imesema kuwa imewakamata viongozi hao katika nyakati tofauti na kati yao wapo watumishi wa Serikali na Wafanyabiashara.

Imewataja watuhumiwa hao kuwa ni pamoja na Mjumbe wa Baraza la Jumuiya ya Wazazi CCM, Sifael Palangyo, Katibu wa Malezi Wilaya ya Longido, Upendo Ndorosi na Katibu wa Wazazi Wilaya ya Longido, Laraposho Laizer .

Wengine ni Katibu wa Wazazi kata ya Kikatiti Meru, Godwait Mungure Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Tukusi kata ya Loksare Wilayani Monduli Mboiyo Mollel , Mwenyekit wa Kamati ya Pembejeo kijiji cha Tukusi Mikidadi Mollel, Wakala wa pembejeo za kilimo kijiji cha Loit kilichopo Halmashauri ya Wilaya ya Meru Kanankira Mnyari, mfanyabiashara wa Kata ya Oltrumet wilayani Arumeru Gervas Mollel na Joseph Christopher Mollel mfanyabiashara katika Kata ya Oltrumet.

Takukuru imefafanua kuwa, Juni 26 mwaka huu ilipokea taarifa kutoka kwa raia mwema kuwa Lilian Ntoro ambaye anatarajia kugombea Ubunge wa Viti Maalum Wazazi Mkoa wa Arusha alikuwa amempatia fedha Sifael Pallangyo kwa ajili ya kwenda kuwahonga wajumbe wa Baraza la Jumuiya ya Wazazi Walaya ya Longido ili kuwashawishi kumpigia kura katika kura za maoni.

“Baada ya kupokea taarifa hiyo Takukuru Mkoa wa Arusha kwa kushirikiana na Ofisi ya Wilaya ya Longido ambao waliandaa mtego na kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa wanne kila mmoja akiwa na kiasi tofauti cha fedha zilizokuwa zimeandaliwa kugawiwa kwa wajumbe wa baraza la wazazi jumuiya ya Wilaya ya Longido,” imesema taarifa hiyo.

Pia imeeleza katika kosa la pili, inawashikilia watuhumiwa wawili ambao ni Gervas Andrea Mollel na Joseph Christopher Mollel wote ni wafanyabiashara wa Kata ya Oltrumet kwa kosa la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu Sh. milioni 15 kutoka kwa mfanyabiashara mwenzao Advera Kyaruz Mkazi wa Mto wa Mbu Wilayani Monduli.