May 18, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Majeneza yenye miili ya wanafunzi waliokufa kwa kuteketezwa na moto katika Shule ya Msingi Byamungu, iliyopo Kyerwa, Kagera

Vilio vyatawala kuagwa miili ya wanafunzi 10 walioteketea kwa moto

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Kagera

MIILI ya wanafunzi 10 waliokufa kwa ajali ya moto uliounguza bweni la wavulana katika shule ya msingi Byamungu iliyopo wilayani Kyerwa mkoani Kagera imeagwa leo na kukabidhiwa kwa wanafamilia tayari kwa mazishi.

Kuagwa kwa miili hiyo kumehudhuriwa na viongozi mbalimbali, wakiongozwa na Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dkt. Bashiru Ally, ambaye alimwakilisha Rais John Magufuli pamoja na ummati mkubwa wa waombolezaji.

Akizungumza wakati wa kuagwa kwa miili hiyo, Dkt. Bashiru amewapa pole wafiwa na jamii nzima iliyoguswa na msiba huo akiwasihi wafiwa kuwa na subira katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo, huku akiitaka Serikali pamoja na vyombo vya usalama kuendelea kufanya uchunguzi ili kubaini chanzo cha moto huo.

Katibu mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dkt. Bashiru Ally (wa kwanza kushoto) akitoa heshima za mwisho kwa marehemu waliofariki kwa ajali ya moto septemba 14 mwaka huu.

Dkt.Bashiru ameitaka Serikali na viongozi wa Mkoa wa Kagera kusimamia maagizo aliyoyatoa Rais Magufuli alipokuwa Bukoba na kuwataka wamiliki wa shule kuendelea kutoa ushirikiano pale watakapohitajika.

“Rais Magufuli ameniagiza nije hapa kuwapa pole kwa msiba huu mkubwa, lakini ameniagiza pia kuweka msisitizo wa maagizo yake aliyoyatoa ili kuhakikisha mazingira ya watoto wetu wanapokuwa shuleni yanakuwa salama.” Amesema Dkt. Bashiru.

Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa Kagera Brigedia Jenerali Marco Gaguti, amesema Serikali imekuwa bega kwa bega na wana Kyerwa na hasa wafiwa kwa kuhakikisha marehemu wanahifadhiwa vizuri pamoja na majeruhi wanatibiwa.

Miili ya wanafunzi 10 waliokufa kwa ajali ya moto shule ya msingi Byamungu iliyopo wilayani Kyerwa ikishushwa kwenye gari kwa ajili ya kuombewa dua na sala pamoja na heshima za mwisho.

Amesema tayari zimeundwa kamati za uchunguzi kwenye shule zote za bweni mkoani kwa ajili ya kuangalia miundombinu.

Gaguti ameongeza kuwa kwenye msiba huo Serikali imegharamia gharama zote za mazishi ya wanafunzi waliofariki na gharama za kusafirisha mili pamoja na kuwagharamia majeruhi waliopo hospitalini.

“Sisi kama Serikali tayari tumeshaanza kuchukua hatua, wapo majeruhi 6 ambao wapo hospitalini ambapo watano wapo Bugando Mwanza na mmoja yupo hapa hospitali ya mkoa, majeruhi hao watatibiwa kwa gharama za Serikali na kwa familia zilizopoteza wapendwa wao Serikali inatoa ubani wa 270,000 kwa kila familia,” amesema Gaguti.

Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (MNEC) awewasihi wana Kyerwa na wafiwa kutokutumia nafasi hii ya msiba kuanza kuzushiana na kuleta maneno ambayo yanaweza kuleta uvunjifu wa amani.

Amesema katika janga hilo wazazi na wafiwa hawatakiwi kumnyoshea kidole mmiliki wa shule, kwani amekuwa akiishi na watoto wao kwa upendo mkubwa hivyo ajali hiyo imetokea kwa bahati mbaya kama majanga mengine.

Sheikh wa Mkoa wa Kagera, Alhaj Kharuna Kichwabuta amesema kuwa hali hiyo wanadamu wanatakiwa kuipokea kwa kuwa mpangajiwa kila ajali na tatizo kwa mwanandamu ni Mwenyezi Mungu na hivyo wafiwa wanatakiwa kuwa nasubira ambapo mmiliki wa shule hiyo Abdu Bushagama amemshukuru Rais Magufuli kwa huruma zake.

Usiku wa kuamkia Septemba 14 mwaka huu ilitokea ajali ya moto katika shule ya msingi Byamungu ambapo bweni la wavulana kwenye shule hiyo liliuungua na kusababisha vifo vya watoto 10 na wengine kujeruhiwa.