May 10, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Vijana waaswa kujitolea na kuwa chachu wa kutafuta suluhu

Na Mwandishi wetu,Timesmajira online

MRATIBU wa Taasisi isiyo kuwa ya Kiserikali ya My Legacy Amina Ally amewaasa vijana kujitolea na kuwa chachu wa kutafuta suluhu na chan gamoto zilizopo katika jamii zao .

Ally ametoa wito huo jijini Dar es salaam leo Februari 9 , wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kazi zinazofanywa na Shirika hilo.

Amesema Shirika hilo limekuwa likifanya kazi katika jamii ili kutokomeza umasikini na kuishi maisha yenye staha.

Akitaja maeneo ambayo Shirika hilo limekuwa likifanya kazi ya uwezeshaji wa wanawake, vijana kiuchumi na Uongozi shirikishi pamoja utetezi wa haki za wanawake na watoto.

“Lengo kuu la Shirika letu ni kufanya kazi na makundi mbalimbali katika kuhakikisha jamii zinapata ujuzi wa kuweza kutatua chagamoto mbalimbali walizonazo katika jamii zao,”amesema.

Mratibu huyo programu ameendelea kueleza kuwa kupitia programu ya uongozi shirikishi ( kujitolea) wamekuwa wakifanya kazi na Makundi mbalimbali ikiwemo watoto hasa waliopo shule kupitia vilabu vilivyopo shuleni .

Amesema pia taasisi hiyo ya My Legacy imetoa elimu ya ujuzi kwa wanafunzi kupitia klabu zao za shule, kuhakikisha jamii zinaishi maisha ya staha na zinatokomeza umaskini.-Ujuzi wanaofundishwa ni kutengeneza batiki, sabuni, kupanda miti ya matunda, miti ya kivuli, bustani za mboga mboga na kutengeneza sodo.

Kundi lingine ni vikundi katika jamii ikiwemo vya watu wenye ulemavu, pamoja na wataalamu mbalimbali kutoka sekta ikiwemo usimamizi wa miradi.Hata hivyo amesema Taasisi hiyo imekuwa ikifanya kazi na wanafunzi waliopo vyuoni na waliomaliza kutokana na wengi wao wamekuwa hawana ujuzi unaohitaji kwenda kujipatia ajira.

“Tumekuwa tukipokea vijana kutoka vyuoni waliopo na waliomaliza wengi wanapotoka chuo mara nyingi wamekuwa hawana ujuzi unaohitaji kwenda kujipatia ajira hivyo tumekuwa tukiwapokea na kufanya nao kazi kwa kuwapatia ujuzi ili pale watakapo pata kazi sehemu nyingine waweze kutumia ujuzi walioupata kwa kuleta maendeleo,”amesema Ally

Aidha amesema Taasisi hiyo inaamini katika kufanya kazi kwa kujitolea, kwa pamoja kwa kushirikiana kunaweza kuleta mabadiliko hasa katika jamii na kuondoa chagamoto zinazoikabili ikiwemo masuala ya usafi, haki za wanawake na watoto.

“Kupitia rasilimali watu kwa pamoja tunaweza kusaidia kuja na bunifu ambazo zitasaidia kutengeneza programu na Suluhu katika jamii, “amesisitiza.

Kwa upande wa wanufaika wa mafunzo kutoka Taasisi hiyo wameipongeza kwa kuwapatia mafunzo ambayo yameweza kuleta mabadiliko kwao na katika jamii anayoishi.Ally Yusuph, Katibu wa Taasisi ya Green beach amesema Shirika hilo limewezesha kuwaunga mkono kwa kiasi kikubwa katika kikundi chao ambacho kimejikita katika kufanya kazi za kujitolea.