May 21, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kamati ya kudumu ya Bunge ya Afya na UKIMWI yapewa mafunzo

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania, Wizara ya Afya pamoja na NHIF wametoa Semina kwa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Afya na UKIMWI kuhusu maswala mbalimbali ya Bima ya Afya hususan utekelezaji wa sheria ya Bima ya Afya kwa wote.

Kwa upande wake TIRA ilijikita katika upande wa Sheria ya Bima ya Afya kwa wote (UHI) iliyosainiwa Mwezi Novemba na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ambapo sheria hiyo imeipa jukumu la kusimamia undeshaji wa bima hiyo.

Awali akitoa wasilisho kwa niaba ya Kamishna, Meneja Ubora na Udhibiti Vihatarishi Ndg. Zakaria Muyengi amesema kuwa TIRA ina uzoefu wa kusimamia Skimu za bima ya afya kwani tayari TIRA inasimamia Kampuni Saba za Bima zinazojishughulisha na utoaji wa Bima ya Afya.

Aliongeza kwa kusema kuwa tayari TIRA ipo kwenye maandalizi ya kutekeleza jukumu hilo na kwamba kwa sasa imeshaunda timu inayopitia na kuandaa muundo wa TIRA ili kuweza kunzisha Idara maalum itakayoshughulikia maswala ya UHI.

Akijibu maswali ya wajumbe wa kamati hiyo ya Afya na Maswala ya Ukimwi Kamishna wa Bima Dkt. Baghayo Saqware amesema TIRA itatekeleza ipasavyo majukumu iliyokasimiwa kwa mujibu wa sheria na kwamba itatumia uzoefu iliyokua nao katika kusimamia sekta ya Bima ili kuboresha sekta ya afya nchini. Kamishna pia amepokea ushauri uliotolewa na wajumbe kuhusu utekelezaji wa sheria ya Bima ya Afya kwa Wote.