May 10, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Tanzania kuanzisha ndege ya moja kwa moja mpaka Poland

Na Penina Malundo,Dar es Salaam

TANZANIA na Poland zimejadiliana na kukubaliana kushirikiana katika sekta za kimkakati ambazo zitawezesha kuimarisha uhusiano wa kiuchumi ikiwemo kuanzisha safari za ndege za moja kwa moja kutoka Tanzania hadi Poland .

Hayo yamesemwa na Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan na Rais wa Poland Andrzej Duda wakati wakizungumza na waandishi wa habari leo Ikulu jijini Dar es Salaam.

Amesema wamekubaliana mambo mbalimbali katika ujio wake ambapo utaenda kukuza sekta ya Utalii,Uwekezaji,Afya pamoja na mambo ya Tehama ambapo wao ni wataalamu katika mambo hayo.

“Ili kuchochea zaidi utalii na biashara hapa nchini wataalamu wameelekezwa kuchukua hatua zitakazo wezesha  kuanza safariza ndege kutoka Poland hadi Tanzania moja kwa moja tumeweka ombi letu kwa ukubwa nchini Poland, “amesema Dk. Samia. 

Amesema Poland  ni miongoni  mwa nchi 10 ambazo raia wake hutembelea Tanzania  kwa wingi kwa shughuli za utalii. 

Amesema wamekubaliana na Rais Andrzej  Duda kuimarisha  ushirikiano  uliopo na kuhamasisha uwekezaji zaidi  kwenye sekta za mikakati  kama vile viwanda, madini gesi asilia na uchumi wa buluu.

Wanaendelea kuimarisha uhusiano kati ya  Tanzania na Poland katika sekta mbalimbali ikiwemo  kilimo, elimu,  uwekezaji,  utalii, viwanda,  uchumi wa buluu na TEHAMA,”amesema.

Rais Samia amesema Poland imekuwa na mchango mkubwa katika uchumi wa Tanzania ambapo watalii 41,000 wamekuja nchini, huku katika kipindi cha mwezi Januari 2024 watalii 6,000 kutoka Poland wamekuja.Rais Samia amesema pia Tanzania na Poland zitaendelea kushirikiana kwenye sekta ya elimu na afya ambapo Watanzania watapata fursa ya kujifunza zaidi.
“Poland ipo tayari kutoa bima kwa benki za biashara kupitia Wakala wa Mikopo wa Usafirishaji kwa ajili ya utekelezaji mradi wa reli ya kisasa kwa vipande vya Makutupora hadi Tabora na Tabora hadi Isaka,” amesema.

Aidha amewakaribisha wawekezaji hususani wa utalii  kuja kuwekeza katika ujenzi  wa mahoteli nchini kwani  kuna maeneo mazuri  ya uwekezaji  katika uzalishaji. 

Amesema masuala ya biashara uhusiano bado ni mdogo hivyo inabidi kuongeza kasi ili kukuza biashara kati  ya nchi hizo mbili.

Kwa Upande wake  Rais wa Poland,  Andrzej Duda amesema ziara yake nchini imelrnga kuibua maeneo mapya ya ushirikiano kati ya nchi hizo mbili na kuleta faida mbeleni. 

Amesema  wamekuwa na uhusiano wa miaka 62 na Tanzania na kuimarisha uhusiano wao tangu vita ya pili ya dunia.

Nitaimarisha uhusiano katika sekta ya utalii na watalii kuendelea kuongeza kuja kutembelea Tanzania na kushawishi wawekezaji kuja kuwekeza Tanzania kutoka Poland,”amesema Rais Duda.

Rais wa Poland yupo nchini kwa ziara ya siku mbili kuanzia Februari 8 hadi 9 mwaka huu.