Na Joyce Kasiki, Dodoma
MAMLAKA ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) imebuni kifaa maalumu (LUGOBO) kinachorahisisha uvunaji wa parachichi na matunda mengine bila kupanda miti au kuyapiga hatua inayolenga kuongeza ubora wa mazao, kupunguza ajali kwa wakulima na kuongeza thamani ya mazao ya bustani.
Akizungumza katika Maonesho ya Nanenane yanayofanyika jijini Dodoma, Mkufunzi wa VETA Mkoa wa Mbeya Mhandisi Anthony Liochi, anesema kifaa hicho kimeundwa kwa lengo la kutatua changamoto zinazowakabili wakulima wakati wa kuvuna matunda kama parachichi, maembe na machungwa.
Anesema kifaa hicho kina kikapu maalumu kinachopokea tunda mara tu linapokatwa kutoka mtini, hivyo kuzuia tunda kuanguka chini na kuharibika au kupoteza ubora wake.
“Kifaa hiki kinamwezesha mkulima kuvuna matunda kwa urahisi bila kupanda mti. Hivyo kinapunguza hatari ya kuanguka, lakini pia kinahifadhi ubora wa tunda kwa sababu halianguki chini,” amesema Liochi.
Aneeleza kuwa katika uvunaji wa kawaida, wakulima wengi hulazimika kupanda miti au kutumia mawe na vifaa visivyo salama, hali inayoweza kusababisha ajali pamoja na kuharibu matawi ya miti na kuathiri uzalishaji wa msimu unaofuata.
Kwa mujibu wa Liochi, matumizi ya kifaa hicho yanasaidia kulinda afya ya mkulima, kuhifadhi miti na kuhakikisha matunda yanavunwa katika ubora unaokubalika sokoni, jambo linaloweza kuongeza kipato cha wakulima.
Amesema kwa sasa kifaa kilichopo ni mfano wa maonesho unaotumika kuwaonesha wananchi namna teknolojia hiyo inavyofanya kazi, huku VETA ikiwa tayari kukitengeneza kwa mahitaji ya mkulima yeyote atakayehitaji baada ya kuwasiliana na chuo.
“Tunatumia maonesho haya kuwafikia wananchi na kuwaonesha namna kifaa hiki kinavyofanya kazi. Baada ya maonesho, tutatoa mawasiliano yetu ili wakulima wanaohitaji waweze kuagiza kifaa kulingana na mahitaji yao,” alisema.
Aidha, anewahimiza wakulima na wadau wa sekta ya kilimo kutembelea banda la VETA katika Maonesho ya Nanenane ili kujionea teknolojia mbalimbali zinazobuniwa na taasisi hiyo kwa lengo la kuongeza tija, usalama na thamani ya mazao ya kilimo nchini.
Amesisitiza kuwa ubunifu wa teknolojia za ndani ni sehemu ya mchango wa VETA katika kuhamasisha matumizi ya teknolojia rahisi na nafuu zinazoweza kutatua changamoto za wakulima na kuongeza ushindani wa mazao ya Tanzania katika soko la ndani na nje ya nchi

More Stories
Mwanafunzi abuni Lishe Bora kupambana na utapiamlo
VETA yaleta suluhisho uharibifu wa Parachichi
Mahundi awataka vijana kukemea uchochezi na kuitetea serikali