August 4, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Makampuni ya Bima yaunganisha nguvu kulinda kilimo Tanzania

Na Joyce Kasiki, Dodoma

UMOJA wa Makampuni ya Bima Nchini (TAIC) umewataka wakulima na wafugaji nchini kujiunga na bima ya kilimo ili kulinda mazao na mifugo dhidi ya majanga mbalimbali yanayosababisha hasara na kupunguza uzalishaji.

Akizungumza jijini Dodoma, mwakilishi wa TAIC amesema makampuni 15 ya bima yameungana kuunda umoja huo kwa lengo la kutoa huduma ya bima ya kilimo kwa pamoja, hatua inayolenga kuongeza uwezo wa kukabiliana na athari za majanga yanayoikumba sekta ya kilimo.

Amesema hapo awali kila kampuni ilikuwa ikitoa bima ya kilimo kivyake, lakini kutokana na ongezeko la majanga yanayohusiana na kilimo na mifugo, makampuni hayo yaliona umuhimu wa kuunganisha nguvu ili kushirikiana katika kutoa huduma hiyo kwa ufanisi zaidi.

“Tupo hapa kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa bima ya kilimo na kuwahamasisha wakulima pamoja na wafugaji kulinda mazao na mifugo yao kupitia huduma hii,” amesema.

Amefafanua kuwa bima ya kilimo huwapa wakulima na wafugaji utulivu wa kuendelea na uzalishaji hata wanapokumbwa na majanga kama magonjwa ya mifugo, mafuriko, mvua nyingi au ukame, kwani hupunguza athari za kifedha zinazoweza kujitokeza.

Aidha, amesema uwepo wa bima huchangia kuongeza uzalishaji na tija kwa kuwa wakulima na wafugaji hupata uhakika wa kuendelea na shughuli zao bila hofu ya kupoteza uwekezaji wao kutokana na majanga yasiyotarajiwa.

TAIC imewahimiza Watanzania, hususan wakulima na wafugaji, kutumia huduma za bima ya kilimo kama njia ya kulinda uwekezaji wao na kuchochea maendeleo ya sekta ya kilimo nchini