March 29, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Uwekezaji wa Benki ya CRDB kwenye kilimo

Na Yusuph Mussa, Mbeya

BENKI ya CRDB imekuwa kwenye jitihada za kuwasaidia wakulima kupata mikopo ili kuweza kulima kwa tija, na kuweza kuinuka kiuchumi, ambapo katika mwaka wa fedha wa 2021/2022 imetoa jumla ya mikopo ya kilimo inayofikia sh. bilioni 769 sawa na asilimia 43 ya mikopo yote ya kilimo inayotolewa na mabenki hapa nchini.

Kati ya mikopo hiyo, sh. bilioni 494i imeelekezwa kwenye mazao makuu ya kimkakati hivyo kusaidia zaidi ya vyama vya ushirika (AMCOS) 472 kupata mikopo kwa ajili ya kuongeza tija kwenye uzalishaji wa kilimo ikiwemo mikopo ya pembejeo, maghala, ujenzi wa viwanda vya kuchakata mazao, mikopo kwa ajili ya miradi ya ufugaji, uwekezaji kwenye misitu na mazao yake pia uwekezaji kwenye uvuvi.

Hayo yalisemwa Agosti 8, 2022 na Meneja Mwandamizi wa Kilimo Biashara Benki ya CRDB Shaaban Maregesi, alipokuwa anazungumza na mwandishi wa habari hizi kwenye Maonesho ya Nane Nane Kitaifa yanayofanyika mkoani Mbeya, ambapo kwa kipindi cha miaka mitano ilyopita hadi kufikia mwezi Juni 2022, Benki ya CRDB imetoa mikopo kwenye sekta ya kilimo inayofikia kiasi cha sh. trilioni 2.6

“Benki ya CRDB ndio Benki pekee ya biashara iliyoanza kutoa mikopo nafuu zaidi kwenye sekta ya kilimo kwa riba ya asilimia tisa tu kwa mwaka. Hali hii imechagiza uwekezaji kwenye sekta ya kilimo na hivyo kukuza uchumi wa nchi kupitia ajira na Pato la Taifa kwa ujumla.

“Wakulima wadogo wadogo kupitia kwenye vyama vya ushirika wanaunganishwa na mifumo madhubuti ya kifedha kupitia mtandao imara wa Benki ya CRDB. Mkulima anaweza kupata huduma za kifedha kupitia CRDB, wakala na simu za mkononi, hivyo kujijengea tabia za kujiwekea akiba kupitia huduma rahisi zinazopatikana hadi vijijini.” alisema Maregesi.

Maregesi alisema Benki ya CRDB iko mstari wa mbele katika kufanikisha miradi mikubwa ya kimkakati benki imeweza kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa Mradi wa Umeme wa Gesi – Kinyerezi Awamu ya kwanza na ya Pili ya MW 150. Pia usambazaji wa umeme vijijini kupitia REA, Mradi wa Umeme wa Mwalimu Nyerere Hydro – MW 2,115, upanuzi wa viwanja vya ndege. ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) Dar es Salaam-Morogoro-Dodoma-Tabora hadi Mwanza.

Ujenzi wa Barabara Kuu zinazo unganisha mikoa na wilaya zote za Bara na Visiwani kupitia wakandarasi mbalimbali wanaopewa kazi za ujenzi wa miundombinu hii muhimu.
Ujenzi wa miundombinu ya maji na usambazaji wa huduma muhimu ya maji mijini na vijijini kupitia mamlaka za maji za mikoa.

Benki ya CRDB imekuwa mstari wa mbele katika kufufua ushirika kwa kuongeza mitaji ili kuhuisha na kuujenga ushirika imara na imeweza kutoa mtaji wa sh. bilioni 3.2 kwa TACOBA na bilioni saba kwa KCBL, hivyo kuwezesha benki hizo za ushirika kupata mtaji unaofikia kiasi cha sh. bilioni 10.2

“Tunatoa wito wa kuvikaribisha vyama vyote vya ushirika nchini kujiunga na Benki ya CRDB ili viweze kujikwamua kiuchumi na kupata mazingira wezeshi kwenye sekta zote za kiuchumi. Benki ya CRDB ina utaratibu mzuri wa kuwaunganisha wakulima na wanunuzi wa mazao yao ndani na nje ya nchi.
Wakulima wengi wamekuwa hawatumii pembejeo sahihi katika uzalishaji wa mazao ya kilimo na hivyo kupata mavuno hafifu, gharama kubwa za uzalishaji na kupata faida kidogo.

“Hali hii hupunguza kasi ya ukuaji wa sekta ya kilimo na uchumi kwa ujumla. Benki ya CRDB inatoa mikopo kwa ajili ya ununuzi wa pembejeo kwa jumla (bulk procurement). Utaratibu huu umesaidia sana kupunguza gharama za upataikanaji wa pembejeo kwa wakulima nchini. Wanunuzi wakubwa wa pembejeo wanaweza kuagiza pembejeo kupitia LC ambazo hutozwa gharama isiyozidi asilimia nne (4%) tu kwa mwaka” alisema Maregesi.

Alisemq Benki ya CRDB ikishirikiana na Wizara ya Kilimo kupitia TFRA imefanikiwa kubuni mfumo madhubuti wa kidigitali ili kurahisisha usambazaji wa mbolea za ruzuku.

Benki ya CRDB ikishirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, inaendelea kuwawezesha wajasiriamali wa awali, wa kati na wakubwa walioko Unguja na Pemba kupitia mpango maalum wa Inuka na Uchumi wa Buluu kwa kutoa mikopo ili waweze kuongeza mitaji yao kwenye shughuli za kilimo, uvuvi, ufugaji na biashara. Katika mpango huu, zaidi ya sh. bilioni. 60 zitatolewa kwa wanufaika wasiopungua 50,000 walioko Zanzibar ili waweze kuongeza mitaji kwenye miradi yao na kuongeza tija kwenye uchumi wa nchi.

Benki ya CRDB pia inao mpango madhubuti wa utoaji mikopo maalumu ya zana bora za kilimo kwa kushirikiana wa wadau wa usambazaji ikiwa ni pamoja nai ETC Agro (Mahindra), LonAgro (John Deere) na Agricom (Kubota & Swaraj). Mikopo hii maalumu inalenga kuwainua wakulima na kufungua fursa kwa kuwawezesha kwa;
Kuondoa masharti ya dhamana ambapo zana za kilimo zitakazonunuliwa kupitia utaratibu huu, ndio zitakuwa dhamana kuu ya mkopo.

Kuweka utaratibu maalumu wa malipo ya mkopo kwa kulinganisha muda wa kuuza mazao na rejesho la mkopo husika. Huduma rafiki baada ya mauzo kwa kupitia wadau wetu ambao wana mtandao mpana nchini kote, kuchangia kidogo kwa kutoa asilimia 25 ya thamani ya mashine itakayo nunuliwa na benki itaweza kutoa mkopo wa asilimia 75 inayobakia, kutoa waranti katika mashine zote kwa muda usio pungua miaka miwili hivyo kuhakikisha mteja anapata zana bora na imara za kilimo.

Moja ya trekta lililopo kwenye banda la Benki ya CRDB kwenye Maonesjo ya Nane Nane mkoani Mbeya. Benki hiyo inakopesha wakukima kwa ajili ya kujishughulisha na kilimo, na mkulima analipa fedha taslimu asilimia 25 ya pesa yote, na iliyobaki inalipwa taratibu kama mkopo. (Picha na Yusuph Mussa).
Moja ya trekta lililopo kwenye banda la Benki ya CRDB kwenye Maonesjo ya Nane Nane mkoani Mbeya. Benki hiyo inakopesha wakukima kwa ajili ya kujishughulisha na kilimo, na mkulima analipa fedha taslimu asilimia 25 ya pesa yote, na iliyobaki inalipwa taratibu kama mkopo. (Picha na Yusuph Mussa).
Wakulima wakiangalia moja ya trekta lililopo kwenye banda la Benki ya CRDB kwenye Maonesjo ya Nane Nane mkoani Mbeya. Benki hiyo inakopesha wakukima kwa ajili ya kujishughulisha na kilimo, na mkulima analipa fedha taslimu asilimia 25 ya pesa yote, na iliyobaki inalipwa taratibu kama mkopo. (Picha na Yusuph Mussa).
Baadhi ya wananchi walifika katika banda la Benki ya CRDB kwenye Maonesho ya Nane Nane mkoani Mbeya. Benki hiyo inakopesha wakukima kwa ajili ya kujishughulisha na kilimo, na mkulima analipa fedha taslimu asilimia 25 ya pesa yote, na iliyobaki inalipwa taratibu kama mkopo. (Picha na Yusuph Mussa)