December 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Uvuvi kuja na mkakati kitaifa kukuza zaidi uchumi

Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza

BAADA ya Taifa kuingia kwenye uchumi wa kati, Wizara ya Mifugo na Uvuvi imekuja na mradi wa kitaifa wa kuaanda mpango kabambe wa kuendeleza sekta ya uvuvi ili iweze kuchangia zaidi kwenye uchumi.

Akizungumza kwenye ufunguzi wa mkutano wa kikanda wa wadau wa sekta ya uvuvi Kanda ya Ziwa wa maandalizi ya kuandaa mpango kabambe wa uvuvi wa miaka 15 ijayo uliofanyika Mkoani Mwanza, Mkurugenzi wa Uvuvi, Wizara ya Mifugo na Uvuvi Magese Bulayi, amesema tangu mwaka 2015 baada ya mpango kabambe awamu ya kwanza kuisha muda wake wa utekelezaji, Serikali kupitia Wizara hiyo imekuwa ikitafuta wafadhili ili kuweza kufanya mapitio na kuandaa mpango mpya.

Mpango huo ni hitaji muhimu kwa kuwa kumekuwepo na mabadiliko mbalimbali ya kisekta, kiuchumi, kijamii, kiteknolojia na kimazingira ambayo yanahitaji kuwa na mpango unaoendana na wakati husika.

Bulayi amesema, kwa juhudi za Serikali zimefanikiwa ambapo mwaka 2019, shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa mataifa(FAO) walikubali kutoa msaada wa jumla ya milioni 448.5 kwa ajili ya mradi wa kuwezesha kuaanda mpango kabambe wa kuendeleza sekta ya uvuvi ambapo mkataba wake ulisaini Julai,2019 na unatarajia kukamilika Machi 2021.

Serikali ilipata dola za kimarekani 50,000 kutoka benki ya dunia kupitia mradi wa usimamizi shirikishi wa rasilimali za uvuvi Kusini Magharibi mwa Bahari ya Hindi (SWIOFish).

“Mpango kabambe wa kuendeleza sekta ya uvuvi uliondaliwa mwaka 2002 uliisha muda wake wa utekelezaji mwaka 2015 na leo tunajivunia matunda mbalimbali yanayotokana na utekelezaji wake ikiwemo kuimarisha miundombinu ya uvuvi kwa kujenga masoko ya kimataifa ya samaki la Kirumba(Mwanza) na Ferry (Dar es Salaam) ni ukweli usiopingika kuwa leo hii masoko hayo yamekuwa msaada mkubwa kwa jamii za uvuvi,wafanyabiashara na taifa kwa ujumla hili kuendelea kuimarisha ndio maana tumekuja na mradi huo,” amesema Bulayi.

Pia amesema kuwa, sekta ya uvuvi ina mchango mkubwa katika maendeleo ya kijamii na uchumi kwa taifa kwa ujumla kwa kutoa ajira, kipato na fedha za kigeni ambapo kwa sasa inachangia takribani asilimia 1.7 na wananchi wapatao 202,053 wameajiriwa moja kwa moja huku zaidi ya wananchi milioni 4.5 wanategemea shughuli za uvuvi zikiwemo biashara ya samaki katika maisha yao pia ina mchango muhimu katika usalama wa chakula na lishe hususani kwa jamii zinazoishi maeneo ya vijijini ambapo kwa sasa sekta inachangia takribani asilimia 30 ya protini itokanayo na wanyama,” amesema Bulayi.

Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Sera na Mipango, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Joseph Kiraiya akizungumza kwenye warsha ya kikanda wa wadau wa sekta ya uvuvi Kanda ya Ziwa wa maandalizi ya kuandaa mpango kabambe wa uvuvi wa miaka 15 ijayo, uliofanyika Mkoani Mwanza. (Picha na Judith Ferdinand)

Kwa upande wake Mratibu Taifa wa Mradi huo Didas Mtambalike, amesema tayari wameeandaa taarifa za awali ambazo zimepita mule mule kwenye masoko ambayo ni mafanikio ya mradi wa awali huku ujenzi wa maabara ya kupima ubora wa samaki ya Nyegezi ikiwa ni faida nyingine ya mpango kabambe wa kuendeleza sekta ya uvuvi ulioisha mwaka 2015.

“Tunataka kuona sasa hivi tuna viwanda 9 vya samaki ukanda wa Ziwa Victoria,mpango huu utuambie kutokana na rasilimali zilizopo katika miaka 15 tuwe na viwanda vingapi,tumeanza kutazama mbele kwaio tujikite tuongeze idadi ya viwanda na masoko,siyo kitu kibaya Nyakariro likawa soko la samaki la kimataifa kama lilivyo Kirumba,tunakwenda sasa haya masoko tuliokuwa tunayaita ya awali sasa yakawe ya upili kama ilivyo Kirumba na Ferry pamoja na BMU 433 upande wa Ziwa Victoria tunataka ziongezeke zifike zaidi ya 1000 kwani tunataka tuongeze udhibiti wa rasilimali hizo na kila Mtanzania aweze kunufaika nao uvuvi,” amesema Didas.

Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Sera na Mipango,Wizara ya Mifugo na Uvuvi Joseph Kiraiya, amesema uchumi ni kila kitu hivyo kabla ujafanya mpango wowote lazima ujue changamoto zipi ulizonazo na fursa ni zipi ndio maana sekta ya uvuvi imekuja na mpango huo,kwani fursa zipo nyingi ikiwemo mito,maziwa,bahari je wamewekeza kwa kiasi gani, wametumia kwa asilimia ngapi kuhakikisha na uchangiaji wa pato la taifa ni kwa kiasi gani ndani ya miaka mitano uvuvi umechanganya on pato la taifa kama asilimia 1.8 ambayo ni ndogo sana.

Mwakilishi wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa(FAO) nchini Oliva Mkumbo, amesema kuondokana na umaskini ni kuhakikisha watu wanapata chakula chenye lishe,uvuvi ni sekta ambayo imekuwa muhimu kwa FAO kwa vile inajishughulisha na uzalishaji wa chakula ambapo jamii ya uvuvi imekuwa maskini kutokana na mambo mengi ikiwemo ya kisera hivyo mpango huo kambabe uliomba FAO uwasaidie ili kuhakikisha sekta hiyo inaendelea na kuwa na mchango katika taifa kwani bila uchumi hakuna maendeleo.

Mmoja wa washiriki wa warsha hiyo Mwenyekiti Msaidizi wa Ulinzi wa Rasilimali za Uvuvi Mwambao mwa Ziwa (BMU)ya Ikuza Kasenyi Wilayani Muleba Christian Christopher, amesema wavuvi wa eneo hilo wanaishukuru Serikali kwa kuruhusu uvuvi wa nyavu za kuunganisha(double 3) na uzalishaji umeongezeka changamoto iliopo kwao ni ushuru kupanda kutoka 100 hadi 300 gafla kitu ambacho kimeleta msuguano baina yao na Serikali hivyo amekuja kuliwasilisha katika warsha hiyo ili liweze kupatiwa ufumbuzi.