June 18, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Utafiti wafichua mazito sekta ya uvuvi baharini

*Wanawake wafanyabiashara wa samaki wafichua unyanyasaji wa kingono mwambao mwa bahari

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online-Tanga

UTAFITI uliofanywa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) katika mikoa ya Tanga, Lindi na Mtwara umebaini uwepo wa vitendo vya ukatili wa kingono dhidi ya wanawake wanaojihusisha na biashara ya samaki katika mwambao wa bahari ya Hindi.

Wanawake hao wanadaiwa kulazimika kuingia katika uhusiano wa kimapenzi ili kupata samaki au kununua kwa bei nafuu, hali inayochochewa na changamoto za kiuchumi pamoja na kupungua kwa rasilimali za uvuvi kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Hivyo wanawake hao,wameibuka hadharani kuelezea changamoto kubwa ya unyanyasaji wa kingono wanayokumbana nayo katika shughuli zao za kila siku, wakidai kuwa baadhi yao hulazimika kuingia katika uhusiano wa kimapenzi na wavuvi au manahodha wa vyombo ili kupata samaki wa kuuza au kununua kwa bei nafuu.

Wakichangia matokeo ya utafiti uliofanywa na LHRC, baadhi ya wanachama wa Umoja wa Wanawake Wavuvi wanaojihusisha na uchakataji, uanikaji, uchemshaji wa samaki pamoja na shughuli za kilimo bahari, wamesema hali hiyo imekuwa sehemu ya maisha yao ya kila siku na imeendelea kuwanyima haki ya kufanya biashara katika mazingira ya usawa na heshima.

Rehema Juma, mmoja wa wanawake wanaojihusisha na biashara ya samaki, amesema mara nyingi wanawake hulazimika kuvumilia vitendo vya unyanyasaji ili kupata fursa za kununua samaki kutoka kwa wavuvi au katika minada.

“Mimi mwanamke kama nataka nipate samaki sokoni au kwenye chombo cha mvuvi natakiwa niwe na uhusiano yaani niwe na “baby” wangu kwenye chombo,huo ni nyanyasaji mkubwa tunaokumbana nao ukienda kwenye mnada unataka kununua samaki, unaongezewa dau ili ushindwe kuchukua apewe mtu mwingine ambaye yuko kwenye uhusiano,” amesema.

Kwa upande wake, Mwanakombo Ally amesema baadhi ya wanawake wenye uwezo wa kifedha hukosa haki ya kupata samaki kwa sababu upendeleo hutolewa kwa wanawake walio katika uhusiano na wavuvi au manahodha wa vyombo vya uvuvi hivyo huo ni aina ya ukatili wa kijinsia unaoendelea kuwaumiza.

Malalamiko hayo yameibuliwa kufuatia matokeo ya utafiti wa LHRC uliofanyika katika mikoa ya Tanga, Lindi na Mtwara, ukiwa na lengo la kuchunguza athari za mabadiliko ya tabianchi katika sekta ya uvuvi pamoja na haki za makundi yanayotegemea shughuli hizo kwa maisha yao.

Akiwasilisha matokeo ya utafiti huo kwa wavuvi wa Moa, Wilaya ya Mkinga mkoani Tanga, Ofisa wa Haki za Binadamu na Biashara wa LHRC, Clay Mwaifani,amesema utafiti umebaini uwepo kwa vitendo vya ukatili wa kingono vinavyowakumba wanawake wanaofanya biashara ya samaki, hususani wale wanaobeba samaki maarufu kama “bodaboda wa samaki” pamoja na wachuuzi.

Amesema wanawake wengi hulazimika kuingia katika uhusiano ya kimapenzi na baadhi ya wavuvi au manahodha ili kupata upendeleo wa kununua samaki kwa bei nafuu au kupata bidhaa kwa urahisi.

Kwa mujibu wa Mwaifani, hali hiyo imechangiwa pia na kupungua kwa upatikanaji wa samaki katika baadhi ya maeneo kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi, jambo ambalo limeongeza ushindani miongoni mwa wafanyabiashara wa samaki.

“Kuna wakati samaki wanapokuwa wachache, mwenye nguvu zaidi za kifedha ndiye anayewapata. Lakini pia hali hiyo huwatengenezea wengine mazingira ya kuingia katika vitendo vinavyotweza utu wao.

” Tumeshuhudia watu wakilazimika kuwa katika uhusiano yasiyotokana na hiari au kuitwa majina yasiyofaa, yote kwa sababu wanapambania kazi zao,” alisema.

Mbali na changamoto za ukatili wa kijinsia, utafiti huo umeonyesha kuwa mabadiliko ya hali ya hewa yameendelea kuathiri uzalishaji wa samaki na kipato cha wavuvi pamoja na wafanyabiashara wa samaki, hususan wanawake ambao wengi wao wanategemea biashara hiyo kwa ajili ya kuendesha maisha ya familia zao.

Akizungumza kuhusu matokeo ya utafiti huo, Afisa Mkuu wa Uchunguzi wa LHRC, Chrisantus Ndibaiukao, alisema lengo la utafiti huo ni kuibua changamoto zinazowakabili wavuvi na kutoa mapendekezo yatakayosaidia kuboresha mazingira ya kazi na kulinda haki zao.

Alisema moja ya changamoto kubwa iliyobainika ni ukosefu wa ushiriki wa kutosha wa wavuvi katika ngazi mbalimbali za maamuzi, jambo linalowafanya washindwe kutetea maslahi yao na kushiriki kikamilifu katika mipango ya usimamizi wa rasilimali za bahari.

“Tunataka kuona sauti za wavuvi zikisikika zaidi katika michakato ya maamuzi ili kuhakikisha sera na mipango inayowahusu inazingatia mahitaji yao halisi,” alisema.

Aidha, utafiti huo umebaini kuwa mbali na changamoto za kiuchumi, wanawake wengi katika sekta ya uvuvi wanakabiliwa na ukosefu wa mitaji, mazingira magumu ya kazi, ubaguzi pamoja na vitendo vya unyanyasaji vinavyowadhoofisha kiuchumi na kijamii.

Vilevile, ripoti hiyo imeonyesha kuwepo kwa migongano ya maslahi kati ya wavuvi wadogo na taasisi za uhifadhi wa mazingira ya bahari. Wakati wavuvi wakihitaji maeneo zaidi kwa ajili ya shughuli za uvuvi, mamlaka za hifadhi zimeendelea kutekeleza mikakati ya kulinda rasilimali za bahari, hali inayozua changamoto katika matumizi ya maeneo hayo na kuathiri shughuli za wananchi wanaotegemea uvuvi kwa maisha yao.