April 27, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Usimamizi wa REGROW wazidi kuimarishwa

Na Mwandishi wetu, Morogoro

WIZARA ya Maliasili na Utalii inaendelea kuimarisha mikakati yake ya usimamizi wa Mradi wa Kuboresha Usimamizi wa Maliasili na Kukuza Utalii Kusini mwa Tanzania (REGROW) kupitia mafunzo maalum ya kuandaa na kusimamia mpango na rejesta ya viashiria hatarishi katika kufikia malengo ya mradi.

Akifungua mafunzo hayo maalum Mkoani Morogoro, Mkurugenzi wa Sera na Mipango, Wizara ya Maliasili na Utalii, Abdallah Mvungi amesema Wizara imeona umuhimu wa kutoa mafunzo ya usimamizi na kushughulikia vihatarishi ili kuwaongezea uwezo wataalam wake wawe na uwelewa mpana katika kupambana na viashiria hivyo kwenye mradi wa REGROW.

“Mafunzo haya ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuhakikisha mradi huu unafikia malengo kwa maslahi mapana ya Taifa na mwananchi mmoja mmoja, hivyo niwatake washiriki wote mzingatie mafunzo haya ili mkawe mabalozi wazuri katika utekelezaji wa mpango huu”. Amesema Mvungi

Aidha Mvungi amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jitihada mbalimbali kubwa anazochukua katika kuboresha usimamizi wa maliasili na kukuza utalii nchini hususan kusini mwa Tanzania, kupitia mradi wa REGROW.

Akimkaribisha mgeni rasmi, Naibu Msimamizi wa Mradi wa REGROW , Blanka Tengia ameeleza kuwa mafunzo hayo yanayoendeshwa na wakufunzi kutoka Idara ya Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa Serikali (IAGD), Wizara ya Fedha, yanatolewa kwa nadharia na vitendo hali ambayo itawafanya washiriki muweze kupata ujuzi wa kuandaa na kusimamia mpango huo na kutekeleza rejesta ya vihatarishi hivyo kwa ufanisi.

Tengia ameongeza kuwa mradi huu wenye lengo la kuboresha usimamizi wa maliasili na kukuza utalii kusini mwa Tanzania unatekelezwa katika hifadhi za Taifa za kipaumbele za Ruaha, Udzungwa, Mikumi, Nyerere na Hifadhi ya Msitu wa Asili Kilombero kwa mkopo wa masharti nafuu kutoka Benki ya Dunia.