May 21, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Usiku wa madini waupamba mkutano wa kimataifa

Na Agnes Alcardo, Timesmajira Online, Dar es Salaam

WAZIRI wa Madini nchini Malawi, Monica Chang’anamuno amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa juhudi kubwa anayofanya katika kuendeleza Sekta ya Madini nchini.

Chang’anamuno ametoa pongezi hizo katika hafla ya Usiku wa Madini uliyoambatana na utoaji Tuzo kwa wadau mbalimbali wa Sekta hiyo, uliofanyika Jana, waliofanya vizuri ikiwa ni sehemu ya kutambua na kuthamini mchango wao kwenye maendeleo na ukuaji wa sekta.

Akizungumza katika hafla hiyo, Chang’anamuno amesema mazingira halisi yanaonesha kuwa Rais Dkt. Samia anaendelea kufanya juhudi nyingi katika kuendeleza Sekta ya Madini kwa kushirikisha wadau mbalimbali kutoka ndani na nje ya Serikali.

Akielezea kuhusu Mpango wa Wajibu wa Migodi kwa Jamii inayozunguka Mgodi (CSR) , Chang’amuno aliipongeza kwa kuwepo Mpango mzuri unaounganishwa na Sera ya Madini katika kutoa fursa za kiuchumi kwa watanzania kushiriki katika uchumi wa madini.

Aliongeza kuwa, amejifunza mengi kuhusu shughuli za uongezaji na kueleza kuwa ataishauri Serikali ya Malawi kuhusu kuwepo wa Kituo cha mfano katika utoaji mafunzo ya uongezaji uhamani nchini humo kama ilivyo kwa Kituo cha Uongezaji Thamani Madini Tanzania cha TGC.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Anglo Ashanti ambaye mdhamini Mkuu wa hafla ya Usiku wa Madini Terry Strong, akitoa hotuba fupi amesema kampuni hiyo itaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania kwa maendeleo ya sekta ya madini.

Katika usiku huo tuzo zilizotolewa ni, Utunzaji wa Mazingira Migodi, Tuzo ya Ukataji na Uongezaji Thamani Madini, Ulipaji wa Mapato ya Serikali, Uwezeshaji wa Ushiriki wa Wananchi katika Sekta ya Madini, Uwajibikaji wa Kampuni kwa Jamii zinazozunguka Migodi.

nyingine ni Mwanamke bora katika uchimbaji wa madini, Mshindi Bora katika Kujenga na tiuzo maalum kwa mtaalam aliyetoa mchangomkubwa katika sekta ya madini ambapo Kamishna wa Tume ya Madini Prof. AbdulKarim Mruma alipata tuzo kama Mtaalam wa Geoscience katika ukuzaji wa sekta ya madini na maendeleo ya nchi.

Kampuni zilizoshinda katika usiku huo ni pamoja na Twiga Minerals Corporation, Shanta Gold, Ako Group, GGML,Appex resources, Ruvuma Coal Limited, Jitegemee Holding, The Tanzanite Experience na Leminatha Colonel Kabigumila.

Wakati huo huo Miss Tanzania Mwaka 2023, Halima Kopwe alikuwa kivutio katika hafla ya Usiku wa Madini wakati wa Onesho la Vito na bidhaa za mapambo.

Pia, warembo wengine walipata fursa ya kupita jukwaani kuonesha bidhaa za madini ya vito na usonara kutokana na madini mbalimbali yanayopatikana hapa nchini.

Kampuni zilizoonesha madini yake ni pamoja na Gem Point, Gem Tanzanite,Ruvu Gemstone, Tanzania Gemological Centre (TGC) na Facet Gems.