May 20, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Umeme kusambazwa Dodoma kwa nyaya chini ya ardhi

Na Mwandishi Wetu

WAZIRI wa Nishati,  Dkt. Medard Kalemani amesema Serikali inatarajia kuanza ujenzi wa miundombinu ya kusambaza umeme jijini Dodoma kwa kutumia nyaya za chini (underground cables) ili kuufanya mji huo kuwa wa kisasa.

Waziri Dkt. Kalemani alitoa kauli hiyo jijini Dodoma jana wakati akihitimisha hoja yake na kujibu michango ya wabunge waliochangia hotuba yake Bungeni ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka 2020/21.

Alisema itafika wakati nyaya zinazoninginia juu hazitaonekana tena katika Jiji hilo. Alisisitiza kwamba Jiji la Dodoma litakuwa la mfano.  

Wakati huo huo, Wizara ya Nishati kupitia Bajeti ya Mwaka 2020/21 imepanga kutekeleza dhamira ya Serikali ya kuhakikisha inazalisha umeme wa kutosha, wa uhakika na wa gharama nafuu.

Pia wizara hiyo imemelenga kuimarisha shughuli za utafutaji na biashara ya mafuta na gesi asilia pamoja na kuwezesha wananchi kunufaika na rasilimali hizo.

Hayo yalisemwa Bungeni jana na Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani wakati akiwasilisha Bungeni Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka 2020/21.

Alisema katika mwaka 2020/21, Wizara ya Nishati inakadiria kutumia jumla ya sh. trilioni 2.197 ikilinganishwa na sh. trilioni 2.142 iliyotengwa kwa Mwaka 2019/20 sawa na ongezeko la asilimia 2.5.

Udhibiti ubora

Aidha Waziri Kalemani alisema Serikali kupitia EWURA imeendelea kusimamia na kuhakikisha miundombinu ya mafuta inajengwa na kuendeshwa kwa kuzingatia viwango stahiki.

“EWURA pia imeendelea kutoa leseni kwa miundombinu ambayo inakidhi viwango ambapo katika kipindi cha Januari 2019 hadi Machi, 2020, imetoa jumla ya leseni 570 za aina mbalimbali na vibali 197 vya ujenzi wa miundombinu ya mafuta,” alisema.

Aidha, alisema EWURA imetoa kibali kwa Kampuni ya Dangote- Mtwara kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha kujaza gesi asilia iliyoshindiliwa kwenye magari (Compressed Natural Gas) ili kuyawezesha magari ya kampuni hiyo kutumia gesi asilia.

Alisema upatikanaji wa mafuta vijijini umeendelea kusimamiwa na kuzipatia ufumbuzi  changamoto zilizopo kutokana na uhaba wa vituo vya mafuta katika maeneo hayo.

Dkt. Kalemani alisema mwaka 2019/20, Serikali imeandaa utaratibu utakaorahisisha uwekezaji katika vituo vya mafuta ambao utapunguza gharama za uwekezaji kwa vituo vya mafuta vijijini ili mafuta yaweze kusambazwa katika njia bora na salama.

“Vilevile, Serikali inaandaa utaratibu utakaorahisisha usambazaji wa gesi asilia na LPG kwa maeneo ya vijijini. Taratibu hizo zinatarajia kukamilika Juni, 2020,”alisema.

Ubora wa mafuta

Dkt. Kalemani alisema Serikali kupitia EWURA imeendelea kusimamia ubora wa bidhaa za mafuta ya petroli zinazosambazwa na kuuzwa nchini.

Katika kipindi cha mwaka 2019, EWURA ilipima sampuli 280 ambapo kati ya hizo, sampuli 30 sawa na asilimia 10.3 hazikukidhi viwango na hatua stahiki za kisheria zilichukuliwa dhidi ya wafanyabiashara waliokutwa na mafuta ambayo hayakidhi viwango.

Alisema njia nyingine inayotumika kudhibiti ubora na ukwepaji wa kodi katika biashara ya mafuta ni uwekaji wa vinasaba (molecular marker) katika mafuta ya petroli, dizeli na mafuta ya taa yanayotumika hapa nchini.

Miradi ya REA

Waziri alisema mradi wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu unalenga kufikisha umeme katika vijiji 7,873. Aidha, alisema hadi kufikia Desemba 2015, jumla ya vijiji 2,018 vilikuwa vimefikiwa na huduma ya umeme.

Alifafanua kwamba idadi hiyo imeongezeka na kufikia 9,112  Aprili, 2020 sawa na ongezeko la vijiji 7,094.

“Vijiji 1,822 ambavyo ni sawa na asilimia 14.86 vitakavyobakia  baada ya Juni, 2020 vitapelekewa umeme kupitia Mradi wa Kupeleka Umeme Vijijini Awamu ya Tatu  Mzunguko wa Pili (Turnkey Phase III – Round II) uliopangwa kutekelezwa katika Mwaka 2020/21,” alisema Waziri Kalemani. Kwa mujibu wa Waziri Kalemani kukamilika kwa mradi huo kutafanya vijiji vyote kufikiwa na umeme.

Alisema kazi zitakazofanyika mwaka 2020/21 ni pamoja na kujenga miundombinu ya kusambaza umeme, kuendelea kusambaza umeme katika maeneo yaliyopo pembezoni mwa mikoa ya Dar es Salaam na Pwani, kusambaza umeme kwenye vitongoji vilivyopitiwa na miundombinu ya usambazaji umeme wa msongo wa kati kupitia mradi wa ujazilizi, kuunganisha wateja na ufungaji wa mifumo ya nishati jadidifu.

Mwenendo wa bei ya mafuta

Akizungumzia eneo hilo, Dkt. Kalemani alisema bei za mafuta katika soko la Dunia zimeendelea kushuka kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo uhitaji na upatikanaji wa bidhaa hii muhimu katika shughuli za kiuchumi.

Alisema wastani wa bei ya mafuta ghafi katika soko la dunia katika mwezi Aprili, 2020 ilifikia Dola za Marekani 23.27 kutoka Dola za Marekani 60.39 kwa pipa mwaka 2019 sawa na punguzo la asilimia 61.5.

“Kushuka kwa bei ya mafuta ghafi katika soko la Dunia kumesababisha kushuka kwa bei ya mafuta yaliyosafishwa ambapo wastani wa bei ya mafuta yaliyosafishwa katika soko la dunia ilikuwa Dola za Marekani 593, 578 na 612 kwa tani kwa mafuta ya petroli, dizeli na mafuta ya taa/ndege mtawalia, ikilinganishwa na wastani wa Dola za Marekani 646, 606 na 575 kwa tani kwa kipindi kama hicho mwaka 2018.

Hii ni sawa na pungufu ya asilimia 8 na asilimia 5 kwa mafuta ya petroli na dizeli mtawalia. Aidha, bei ya mafuta ya taa/ndege imeongezeka kwa asilimia 6,”alisema.