April 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

ULAJI NYANYA CHUNGU UNAVYOSAIDI MAGONJWA YASIYOAMBUKIZA

Na Aveline  Kitomary,TimesMajira online,Dar es Salaam.

LISHE bora ni sehemu muhimu katika afya ya binadamu hasa katika kuimarisha mwili na kulinda na magonjwa mbalimbali hasa magonjwa yasiyoambukiza.

Miongoni mwa lishe inayoshauriwa na wataalamu wa afya ni ulaji wa matunda na mbogamboga kutokana na faida lukuki zinazozopatikana.

Leo katika Jarida la Majira ya Afya tutaangazia kuhusu mmoja wapo la tunda linaloitwa Nyanya chungu au ngogwe ambalo linatumika katika mapishi.

Nyanya chungu au ngogwe (African eggplant) kwa jina la kitaalamu ni Solanum aethiopicum” ni tunda ambalo likipikwa linaweza kuliwa kama mboga kwenye mlo wa kila siku.

 Nyanya chungu vile vile linaweza kuliwa likiwa bichi ama likiwa limekaushwa au likiwa limeokwa.

Tunda hili pia huusishwa kwa ukaribu sana na matunda jamii ya mabilinganya au Eggplant (aubergine).

Licha ya kuongeza ladha katika chakula Nyanya chungu inafaida nyingi katika mwili wa binadamu ambapo tutaziangazia.

CHANZO KIKUBWA CHA VITAMINI NA MADINI MWILINI

Mtaalamu wa lishe kutoka Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania(TFNC)  Fatuma Mwasora anaiambia Jarida la Majira ya Afya kuwa  Nyanya chungu au ngogwe zina umuhimu mkubwa mwilini kutokana na kuwepo kwa madini na vitamini kwa wingi.

Anasema kuwa Vitamini na madini ni virutubishi vinavyohitajika mwilini kwa ajili ya kuukinga mwili dhidi ya maradhi na kuufanya uwe na afya bora.

Anaeleza kuwa Madini na vitamini kwenye nyanya chungu au ngogwe ni muhimu kwani husaidia kuulinda mwili dhidi ya maradhi.

“Mfano wa madini hayo ni pamoja na madini ya chuma, Nyanya chungu au ngogwe ni chanzo kizuri cha madini ya chuma mwilini.

“Uwepo wa vitamini C (ascorbic asidi) kwenye nyanya chungu husaidia katika ufyonzwaji wa madini ya chuma kwa wingi mwilini na  Madini ya chuma ni moja ya kirutubishi muhimu katika utengenezaji wa chembe chembe nyekundu za damu na  pia madini ya chuma ni muhimu katika kusidia kusafirishwa kwa hewa ya oksijeni mwilini,”anabainisha Mtaalamu Mwasora.

Kwa mujibu wa Mwasora Madini ya potasiamu nayo ni muhimu mwilini, kwani husaidia kujenga na kuimarisha misuli ya moyo pamoja na kudhibiti shinikizo la damu na husaidia kuulinda mwili dhidi ya ugonjwa wa kiharusi.

“Madini ya shaba ni muhimu katika uzalishaji wa seli nyekundu za damu ambapo tafiti zinaonesha kuwa madini ya magnesiam ni muhimu katika ukuaji na kuimarisha mifupa dhidi ya dhaifu na inavunjika.

“Tafiti zinaonesha kuwa kuna vitamini nyingi kwenye nyanya chungu au gongwe, ikiwa ni pamoja na vitamini A ambayo huweza kuyeyuka katika mafuta kwa urahisi na hii Vitamin A ni muhimu kwani husaidia kuimarisha mfumo wa kingamwili, kuona vizuri hasa kwenye mwanga hafifu, husaidia kuitengeneza ngozi na kuwa laini na pia husaidia katika ukuaji mzuri wa mwili,”anaeleza Mwasora.

Mwasora anasema kuwa Vitamin B inayopatikana katika nyanya chungu au ngongwe ni muhimu katika ufyonzwaji na utumikaji wa mafuta mwilini.

“Kundi la vitamini B, kwa mfano vitamini B1 (thiamine) na vitamini B3 (Niacin au asidi ya Nikotini) na vitamini B6 nayo inapatikana kwenye nyanya chungu au ngogwe.

“Vitamini K ni muhimu katika kusaidia ugandaji wa damu mwilini Mfano pindi unapopata katika mwili ambalo litapelekea damu kutoka, basi vitamini K husaidia kuhakikisha damu haitoki zaidi katika jeraha na hatimaye damu hukata.

“Tafiti zinaonesha kuwa vitamini K inauwezo mkubwa wa kuzuia ukuaji wa seli za saratani katika mwili wa binadamu na kuimarisha mifupa na pia Vitamini K  hupunguza magonjwa sugu yasiyo ya kuambukiza kama vile magonjwa ya moyo, baadhi ya saratani na ugonjwa wa kupoteza kumbukumbu “Alzheimer’s”.

“Tafiti zinaonyesha kuwa kuwa na vitamini K vya kutosha huzuia ama kupunguza athari za kupata stroke yaani kupalalaizi,”anaeleza Mwasora.

UMUHIMU WA VIONDOA SUMU VILIVYOKO KATIKA NYANYA CHUNGU AU GONGWE

Miongoni mwa faida kubwa ya ngogwe ni ukamilifu wa viondo sumu yaani  “ANTIOXIDANTS” ambavyo hufanya kazi kubwa zaidi katika ulinzi wa mwili dhidi ya magonjwa .

Mwasora anasema kuwa Viondoa sumu “antioxidants” vilivyoko katika nyanya chungu au gongwe ni viini ambavyo vina uwezo wa kuzikinga seli za mwili zisiharibiwe na chembe chembe haribifu (free radicals) ambazo huweza kusababisha magonjwa ikiwemo ugonjwa wa saratani.

“Vile vile kwenye nyanya chungu kuna viini ambavyo huungana na chembe chembe hizo haribifu ili kuweza kuzidhibiti zisisababishe madhara mwilini.

“Kuna aina mbalimbali za viondoa sumu “antioxidants” ambazo kusaidia kuzuia au kupunguza magonjwa sugu yasiyo ya kuambukiza kama vile magonjwa ya moyo na baadhi ya saratani na ugonjwa wa sukari,”anafafanua Mwasora.

Anasema nyanya chungu au ngogwe zina uwezo wa kudhibiti sukari kwenye damu kwa sababu ya makapimlo au nyuzi nyuzi au (fibres) nyingi ambazo husaidia katika umeng’enywaji wa chakula.

“Makapimlo hayo yana umuhimu katika uyeyushwaji wa chakula na kusaidia katika umeng’enywaji na ufyonzwaji wa chakula tumboni, ikiwa ni pamoja na kuzuia mtu kupata choo kigumu (constipation).

“Tafiti zinaonesha kuwa wingi wa makapimlo au nyuzi nyuzi au (fibres) pia husaidia kupunguza kiwango kikubwa cha mafuta ya lehemu yaani (cholesterol) mwilini.

“Tafiti pia zinabainisha  kuwa nyanya chungu au ngogwe zina makapimlo au “fibres” kwa wingi hivyo yanaweza kusaidia kupunguza kiwango cha sukari kwenye damu na  Kuwepo kwa makapimlo kwa wingi na kiwango kidogo cha kalori kwenye nyanya chungu au gongwe kusaidia katika kupunguza uzito.

“Upo utafiti mwingine ambao unaonesha kuwa ulaji wa nyanya chungu mara kwa mara kunaweza kusaidia katika kuulinda mwili na baadhi ya saratani na zingine pia zinaonesha kuwa viini aina ya “solasodine rhamnosyl glycosides, kwenye mimea kama nyanya chungu huweza kusaidia kuulinda mwili dhidi ya baadhi ya saratani,”anaeleza Mwasora.

nyanya chungu zilizopikwa

UMUHIMU WA NYANYA CHUNGU KATIKA KUFANIKISHA KAZI YA UBONGO

Mwasora anabainisha kuwa Tafiti zinaonesha kuwa kwenye nyanya chungu au ngongwe kuna aina ya kemikali za asili zinazoitwa “phytonutrients”, ambazo ni muhimu katika kuboresha afya ya akili.

“Kitendo la kupeleka damu zaidi kwenye ubongo au kuongezeka kwa mzunguko wa damu mwilini, “phytonutrients” husaidia pia kuongeza kumbukumbu kwa kuchochea njia katika “neural pathways” ziweze kukua,”anasema.

MATUMIZI YA NYANYA CHUNGU AU NGOGWE

Mtaalamu huyo wa lishe anabainisha kuwa Nyanya chungu au ngogwe zinaweza kutumika zikiwa mbichi au zilizopikwa. 
 
“Pia zinaweza kuokwa, kukaushwa, kukaangwa, kusagwa na pia kuchanganywa katika mapishi mbalimbali hasa mchuzi. 
 
Mwasora anashauri watu kutumia nyanya chungu ili iweze kuwasaidia na kulinda mwili dhidi ya magonjwa hasa magonjwa ya kuambukiza.
 
“Na ndio maana inashuriwa kula vyakula mchanganyiko kwasababu kuna faida nyingi katika kila unachokula hasa  kama tulivyoona faida ya nyanya chungu au ngogwe ni kubwa zaidi.
 
“Ni yema kutumia  mara kwa mara  katika mlo kutokana na faida zake zilizoainishwa hapo juu kwani ni muhimu zaidi,”anashauri Mwasora. 

Mwishooo….