April 19, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ujenzi wa miundombinu ya Mahakama uendane na huduma za kisheria

Na Hadija Bagasha, TimesMajira Online,Tanga

JAJI Mkuu wa jamuhuri Nchini Uganda Alphonse Owiny – Dollo amesema ujenzi wa miundombinu ya mahakama unaofanywa na serikali unapaswa kuendana na huduma ya kisheria inayotolewa na maafisa wa mahakama.

Jaji huyo ametoa kauli hiyo wakati alipokuwa na ujumbe wake kwenye ziara ya kutembelea chuo cha uongozi wa mahakama IJA kilichopo wilayani Lushoto Mkoani Tanga.

Jaji Mkuu wa Uganda, Owenyi amesema upo umuhimu mkubwa wa kuhakikisha ujenzi wa miumdombinu unaofanywa na serikali unaendana na huduma ya kisheria ili kuweza kuwa na tija kwa jamii.

Aidha alisema yeye pamoja na ujumbe aliouongoza wamejifunza mbinu za kufanyia maboresho taasisi ya Uganda ili iweze kukidhi matakwa ya elimu ya Sheria kwa wananchi wa Uganda na nchi za jirani.

Alisema ziara yao ya siku tatu chuoni hapo imewawezesha kujifunza mambo mengi ambayo wanakwenda kuyafanyia maboresho makubwa.

Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto ( IJA) ambaye pia ni Jaji wa mahakama ya rufani Dkt. Paul Kihwelo alisema licha ya kutoa mafunzo kwa ngazi ya astashahada na stashahada, chuo hicho kimekuwa kikiendesha kozi za kuwajengea uwezo watendaji wa idara ya mahakama nchini wakiwamo majaji.

Dkt Kihwelo alisma mbali ya watendaji wa mahakama alisema IJA pia imekuwa ikiendesha mafunzo ya kuwajemgea uwezo watumishi wa taasisi nyingine za kiserikali na zisizo za kiserikali nchini ambazo zimesaidia kuleta ufanisi kazini.

” Haya mafunzo ya hapa IJA yamewavutia sana wenzetu wa Uganda wakiongozwa na Mheshimiwa Jaji Mkuu wa Uganda kwa sababu yanasaidia kupunguza migogoro kazini na hivyo kupungua kwa kesi zinazowasikishwa mahakamani zihusuzo malalamiko kazini”alisema Jaji Kihwelo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa baraza la uongozi wa chuo cha mahakama IJA ambaye pia ni Jaji wa mahakama ya Rufani Dkt. Gerald Ndika amesema upo umuhimu wa kushirikiana na Uganda ili kuboresha huduma za kimahakama.

Mkuu wa taasisi ya JTI ya Uganda,Jaji Damalie Lwanga alisema kuwa kutokana na ukweli kwamba taasisi yake ni changa ambayo imeanza hivi karibuni kutoa mafunzo kisheria,Uongozi wa Mahakama Uganda umelazimika kifanya ziara Lushoto ili kujifunza na kubadilishana uzoefu na chuo cha IJA.

“Tupo katika mchakato wa kukifanyia maboresho JTI hasa ikizingatiwa kwamba Sheria ya kukiendesha ilipitishwa mwaka jana hapo awali kilikuwa kikiendeshwa na maelekezo ya Jaji Mkuu hivyo tumekuja kujifunza na kubadilishana uzoefu alisema Jaji Lwanga.

Hatua ya ziara hiyo inafuatia maboresho ya mahakama na chuo Nchini Uganda kufuatia sheria ya mahakama iliyotungwa mwaka 2020 nchini humo.

Hata hivyo Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto ( IJA) kimeanza kushirikiana na taasisi ya mafunzo ya Mahakama Uganda (JTI) ili kuboresha sekta ya sheria kwa Tanzania na Uganda.

Mpango wa kubadilishana uzoefu kati ya taasisi ya utawala wa mahakama Lushoto na taasisi ya mafunzo ya mahakama ya Uganda umefanyika katika chuo cha uongozi wa mahakama wilayani Lushoto IJA.