December 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Uingereza yawasomesha watumishi wa Wizara ya fedha.

Na Mwandishi wetu

Watumishi wa Wizara ya Fedha na Mipango, waliopatiwa ufadhili wa masomo katika vyuo mbalimbali nchini Uingereza kwa mwaka 2020/2021 wametakiwa kutumia fursa watakazozikuta kuongeza ujuzi ili kulisaidia taifa watakapomaliza mafunzo yao.

Hayo yameelezwa jijini Dar es Salaam na Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Dkt. Yamungu Kayandabila, kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Doto James wakati wa hafla ya kuwaaga watumishi waliopata ufadhili wa masomo katika vyuo mbalimbali kupitia Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Uingereza (UKaid).

Dkt. Kayandabila alisema kuwa udhamini wa masomo unaotolewa na UKaid umekuwa na faida kubwa kwa nchi kwa kuwa wale waliomaliza mafunzo kwa awamu zilizopita kuaanzia mwaka 2017 wamekuwa na tija na ufanisi katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku na ndio sababu wamepangiwa majukumu mengine mbalimbali.

“Kutokana na umuhimu wa elimu katika maendeleo ya nchi tunaiomba Uingereza kusaidia pia kutoa Kozi za muda mfupi zinazohusiana na Uchumi na Utawala wa Fedha, zitakazoongeza uwezo wa Watumishi wa Wizara ya Fedha na Mipango kuwa na umahiri katika utendaji wa majukumu yao”, alisema Dkt. Kayandabila.

Aidha Dkt. Kayandabila ameipongeza Uingereza kwa jitihada zake za kuisaidia Tanzania katika kuongeza ujuzi, maarifa na ubunifu kwa watumishi jambo ambalo limeongeza uimara wa ushirikiano katika nyanja mbalimbali za maendeleo hasa za kiuchumi.

Kwa upande wake Balozi wa Uingereza nchini Tanzania Mhe. David Concar, alisema kuwa nchini Uingereza kuna fursa nyingi hivyo ni vema watumishi wakazitumia vizuri ili kuongeza ujuzi na ufanisi kwa kusoma kwa bidii na watakaporudi waweze kuisaidia Wizara na wananchi katika masuala mbalimbali yakiwemo ya uchumi, sheria na Sayansi ya Kompyuta.

“Watumishi wa Wizara ya Fedha na Mipango watakaporudi nchini na kuweza kulisaidia Taifa itakuwa ni chachu ya watanzania wengine kuhamasika kwenda kupata ujuzi na maarifa nchini Uingereza”, alieleza Balozi Concar.

 Naye Mkuu wa Programu za Mafunzo wa British Council, Bi. Atiya Sumar, alisema kuwa uwepo wa British Council nchini Tanzania miaka 17 iliyopita kumekuwa na manufaa mengi kati ya nchi ya Tanzania na Uingereza katika ushirikiano, ubadilishanaji wa tamaduni na elimu, ikizingatiwa kuwa ndio mratibu programu ya mafunzo kwa Watumishi wa Wizara ya Fedha kwa awamu zote tano ilizojiwekea kuanzia yalipozinduliwa mwaka 2017.

Nao wanufaika wa mafunzo katika vyuo mbalimbali vya Uingereza akiwemo Bw. Innocenti Lema na Edwin Nalaila, wameishukuru Serikali kwa kufanikisha mafunzo hayo na pia wameahidi kusoma kwa bidi na kutumia fursa zote watakazozikuta ili kuongeza ujuzi na maarifa kwa manufaa ya watanzania.

Wanufaika wa Programu ya Mafunzo katika Vyuo mbalimbali vya Uingereza kwa ufadhili wa UKaid awamu ya nne, kutoka Wizara ya Fedha na Mipango, ni pamoja na Bw. Innocent Lema, Edwin Nalaila, Bi. Paulina Fungameza, William Mhehe na Alpha Temu.

Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Uingereza (UKaid) walizindua programu ya mafunzo kwa watumishi wa Wizara hiyo katika vyuo mbalimbali vya Ungereza kwa ufadhili wa UKaid mwaka 2017, hii ni awamu ya nne ya utekelezaji tangu programu hiyo ianzishwe ambapo watumishi 20 wamenufaika na mpango huo.