May 1, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Uhusiano kati ya Tanzania na nchi mbalimbali waendelea kuimarika

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma

Imeelezwa kuwa Uhusiano kati ya Tanzania na nchi mbalimbali umeendelea kuimarika kutokana na  Tanzania kuendelea kufungua Balozi na Ofisi za Uwakilishi katika nchi mbalimbali za kimkakati.

Hayo yamesemwa jijjji hapa leo,Aprili 18,2024 na Naibu Waziri wa Mambo ya nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,Mbarouk Nassor Mbarouk amesema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio yaliyopatikana katika miaka 60 ya Muungano  Tanganyika na Zanzibar ambapo amesema kuwa lengo  ni sehemu ya kuimarisha utekelezaji wa Sera ya Mambo ya Nje hususan Diplomasia ya Uchumi. 

“Serikali ya Awamu ya Sita imefungua Balozi mpya mbili za Vienna, Austria na Jakata, Indonesia na Konseli Kuu mbili za Lugumbashi na Guangzhou, China. Ufunguzi wa Balozi hizo umeifanya Tanzania kufikisha jumla ya Balozi na Ofisi za Uwakilishi zipatazo 45 na Konseli Kuu tano,”amesema.

Pamoja na hayo,Balozi huyo amesema Tanzania ni mwenyeji wa nchi na mashirika ya kimataifa zaidi ya 90 ikiwemo Konseli Kuu ambazo baadhi yake zipo Zanzibar kama vile China, Oman, India na Umoja wa Falme za Kiarabu. 

“Uwepo wa Konseli kuu umechangia kuimarika kwa ushirikiano wa uwili, ujirani mwema na kuongezeka kwa manufaa katika sekta za ushirikiano ikiwemo biashara, utalii, uwekezaji, uchumi wa buluu na kubidhahisha kiswahili,”amesisistiza

Tanzania imefanikiwa kutoa viongozi mahiri kuongoza taasisi za kikanda na kimataifa ikiwa ni ishara ya kuaminiwa na mataifa mengine ikiwemo uteuzi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kama Mwenyekiti Mwenza wa Mkutano wa Kilele wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia Barani Afrika utakaofanyika Paris, Ufaransa mwezi Mei 2024. 

Aidha, Tanzania pia ilitoa Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ambapo Dkt. Salim Ahmed Salim aliongoza Vikao Vinne vya Baraza  hilo mwaka 1979 na 1980. Vilevile, alihudumu kama Katibu Mkuu wa Umoja wa Afrika (OAU), Dkt. Asha-Rose Migiro kuwa Naibu Katibu Mkuu wa kwanza kutoka Afrika; Balozi Getrude Mongela kuwa Rais wa Bunge la Afrika; Dkt. Stergomena Tax kuwa katibu Mtendaji wa SADC na Balozi Juma Mwapachu katibu Mkuu wa EAC.

Watanzania wengine ni Balozi Liberata Mulamula (Mb), Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu (ICGLR); Profesa Anna Tibaijuka kuwa Naibu Katibu Mkuu na Mkuu wa Shirika la Maendeleo ya Makazi la Umoja wa Mataifa (UN-HABITAT) na Mkuu wa Ofisi za Umoja wa Mataifa Nairobi (UNON), Bi. Joyce Msuya, Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) na hivi karibuni Spika wa Bunge la Tanzania Mhe. Dkt. Tulia Ackson (Mb.) kuchaguliwa kuwa Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), Dkt. Tulia ni mwanamke wa kwanza kutoka barani Afrika kushika wadhifa huo.

Pia amesema Tanzania imechangia katika juhudi za kubidhaisha Kiswahili ndani na nje ya nchi ikiwemo kutoa ushawishi wa matumizi ya lugha hii kama nyenzo ya diplomasia, usuluhishi wa migogoro; ukombozi na uhuru katika nchi za bara la Afrika.

Ambapo kiswahili kuwa lugha rasmi katika Umoja wa Bara la Afrika, Jumuiya ya Afrika Mashariki, Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika. 

Vilevile, Tanzania imefanikiwa kushawishi dunia kupitia UNESCO ambapo imeitambua tarehe 7 Julai kila mwaka kama siku ya Kiswahili duniani. Tanzania kupitia Balozi zake imewezesha kuanzisha madarasa na Vituo vya Kiswahili katika nchi mbalimbali ikiwemo Uholanzi, Ethiopia na Korea Kusini.

Aidha amesema Katika ziara ya  Rais Samia nchini U.A.E, Tanzania imefanikisha kusainiwa kwa Hati za Makubaliano ya Ushirikiano 37 zenye thamani ya Dola za Marekani takribani shilingi billion 8.

“China, imeshuhudiwa utiaji saini wa mikataba na hati za makubaliano ya kimkakati 15 zilizolenga kuimarisha biashara na uwekezaji ambapo China imeisamehe Tanzania deni la thamani ya shilingi bilioni 31.4,”amesema.

Hata hiyyo,Balozi Mbarouk amesema Vilevile, China imeipatia Tanzania msaada wa shilingi bilioni 35.72 na mkopo wa masharti nafuu wa dola za Marekani milioni 56 kwa ajili ya ujenzi wa uwanja wa ndege (Terminal II) Zanzibar.

Kadhalika, kupitia ziara hiyo China imefungua masoko ya parachichi na mabondo ya samaki kutoka Tanzania.