April 29, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Uelewa mdogo chanzo magonjwa ya kinywa, meno

Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza

UTAFITI uliofanywa hivi karibuni umebaini kuwa, uelewa mdogo wa wananchi juu ya magonjwa ya kinywa na meno umesababisha asilimia kubwa ya watu kusumbuliwa na tatizo hilo.

Hayo yamewekwa wazi na Daktari Bingwa wa upasuaji wa shingo, kichwa na meno wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando Dkt. Emmanuel Motega katika zoezi la uchunguzi wa magonjwa ya akina mama ikiwemo saratani ya matiti, meno na kinywa pamoja na mazoezi ya viungo bure kwa wananchi wa Kanda ya Ziwa lililoandaliwa na hospiatali hiyo na kuendeshwa na madaktari bingwa lengo likiwa ni kupambana na changamoto ya magonjwa yanayowakabili wananchi.

Dkt. Motega amesema, kulingana na utafifi uliofanyika unaonesha kuwa asilimia kubwa ya wananchi wana matatizo ya kinywa na meno huku wakiishi na matatizo hayo kutokana na uelewa mdogo walionao hivyo wanatakiwa kuwahi hospitali mara wanapohisi maumivu ya meno au harufu mbaya ya kinywa.

Amesema, kuchelewa kutibia tatizo hilo husababisha bakteria kuingia sehemu nyingine za mwili na kusababisha magonjwa mengine kama ya moyo, kuleta majipu yakashuka kwenye shingoni au kifuani, uvimbe na hata saratani.

“Kwa sasa huduma ya meno imeboreshwa kwa kiwango cha hali ya juu kwani tunaweza kutibu jino bila kung’oa, tunaziba meno, kusafisha fizi ambazo zimepata magonjwa , kufanya upasuaji wa shingo na kichwa,” amesema Dkt.Motega.

Kwa upande wake Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Upasuaji kwenye Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando, Dkt. Vihar Kotecha amesema, Saratani za matiti ni namba tatu kwa saratani zote kwa akina mama hivyo amewasisitiza kuwa na mazoea ya kujichunguza matiti wenyewe kama yana vivimbe.

Dkt. Samweli Byabato ambaye ni Mratibu wa huduma za upasuaji Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando, amewasihi wananchi wote kufanya taratibu za uchunguzi wa afya zao mara kwa mara hasa wajawazito ili kupunguza vifo wakati wa kujifungua.

“Ugonjwa wa saratani unatibika, Hospitali ya Bugando imeboresha huduma kwa upande wa saratani na inatoa tiba ya dawa na mionzi, mwisho wa mwaka huu tumejipanga kufanya uchunguzi wa matatizo ya magonjwa mbalimbali ili kuweza kutatua changamoto zinazowakabili wananchi wengi na kuweza kuwasaidia wagonjwa katika hatua za awali,” amesema Dkt.Byabato.