May 15, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

‘Rais wa Tanga’ jela miaka 30

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Tanga

MAHAKAMA ya Uhujumu Uchumi, imemuhukumu kwenda jela kutumikia kifungo cha miaka 30 mfanyabiashara maarufu Jijini Tanga, Yanga Omari maarufu kama rais wa Tanga baada ya kumtia hatiani kwa kosa la kusafirisha na kuuza dawa za kulevya aina ya Heroin kiasi cha gramu 1052.63.

Mahakama hiyo pia imewaachia huru Mkewe, Rahma Ali na mfanyakazi wake wa ndani Halima Anuwar baada ya upande wa Jamhuri kushindwa kuthibitisha kuhusika na biashara hiyo.

Akitoa hukumu Jaji wa Mahakama hiyo Imakulata Banzi amesema, hukumu hiyo imetolewa baada ya kuridhika na ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka na kumhukumu kifungo hicho.

Hata hivyo, Jaji Banzi amesema, gari aina ya Land-Cruser V8 na silaha yake vilivyokuwa vikishikiliwa na serikali virejeshwe kwa familia huku akitoa amri ya madawa aliyokamatwa nayo yateketezwe mara moja huku pia akizitaka pande hizo mbili kufuata taratibu za kukata rufaa ikiwa hazijaridhika na hukumu hiyo.

Inadaiwa kuwa, Agosti 2018 Yanga, mkewe pamoja na mfanyakazi uyo walikamatwa mtaa wa Bombo Jijini Tanga, wakitaka kusafirisha dawa hizo za kulevya.

Mkurugenzi Msaidizi kutoka ofisi ya Taifa ya mashtaka Faraja Nchimbi ambaye pia anasimamia mashauri mbalimbali ikiwemo masuala yanayohusiana na dawa za kulevya, ugaidi pamoja na masula ya makosa ya baharini amesema kuwa, uamuzi huo ni sehemu ya jitihada ya serikali katika kuhakikisha vita dhidi ya dawa za kulevya inapiganwa vilivyo kwa kuzingatia sheria kali zilizopo.

Kabla ya kutoa hukumu hiyo, Wakili wa upande wa mshitakiwa Mohamed Kajembe, aliiomba mahakama impunguzie adhabu mteja wake, kwasababu ni kosa lake la kwanza na pia ana umri zaidi ya miaka 60, anategemewa na familia kubwa ikiwemo kuwa na tatizo la shinikizo la damu (presha).