August 11, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

UCSAF  yasisitiza ushirikiano na Wahariri

Na Judith Ferdinand, Timesmajira Online- Mwanza 

MFUKO wa Mawasiliano kwa Wote(UCSAF),imesisitiza kuwa uhusiano kati ya mfuko huo na Wahariri wa Habari hapa nchini ni muhimu katika kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi kuhusu miradi ya mawasiliano, maeneo yanayofikiwa na manufaa yake.

Hayo yameelezwa Agosti 10,2026 na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa UCSAF Celina Mwakabwale,wakati wa mafunzo yaliotolewa na mfuko huo kwa Wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari Mkoa wa Mwanza,yaliofanyika wilayani Ilemela mkoani humo.

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa UCSAF Celina Mwakabwale, akizungumza katika mafunzo yaliotolewa na mfuko huo kwa Wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari Mkoa wa Mwanza,yaliofanyika wilayani Ilemela mkoani humo

Ambapo amrsema,Wahariri wa Habari wana nafasi ya kipekee kwa kuwa wanaamua na kuratibu maudhui yanayowafikia wananchi kupitia vyombo mbalimbali vya habari,hivyo uhusiano huo utawezesha habari za UCSAF kupewa kipaumbele kwa maslahi ya umma.

Akiwasilisha mada kuhusu uhusiano baina ya Wahariri wa Habari na UCSAF, Mwakabwale  amesisitiza,umuhimu wa kujenga ushirikiano wa kitaaluma unaozingatia upatikanaji wa taarifa sahihi,uwazi na uwajibikaji,ambao ni msingi wa kuwafikia wananchi wengi zaidi kwa haraka hususani waliokuwa nje ya huduma za uhakika za simu na intaneti.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Mwanza(MPC) Edwin Soko amesema,kupitia mafunzo hayo aliwataka  waandishi wa habari  waweze kuongeza weledi kwenye kazi zao maana  tayari wamejengewa uwezo wa ubobezi katika maeneo ya kuandika habari za wadau.

“Nawasisitiza wawe daraja kati ya UCSAF na jamii,waelimishe jamii wafahamu mfuko huo ni nini,hupatikanaji wa huduma zao upoje na tuwatazame hasa wananchi wa maeneo ya vijijini,”amesema Soko.

Hivyo naamini Wahariri wataenda kutimiza wajibu wao kwa kuandika taarifa zitakazofika kwa jamii na kuelezea uhalisia,umuhimu na utekekalezaji wa mipango ya UCSAF kwa kila mwaka hasa kwenye kuondoa umaskini kwa sababu mawasiliano yakifika sehemu ni uchumi wa kidigitali.

“Bila UCSAF kuwekeza kwenye minara wananchi wanaweza kutengwa na fursa.Waandishi wa habari waende maeneo ya vijijini waibue changamoto hili mfuko huo uone na kutatua,”amesema Soko.

Mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo Mhariri Mkuu wa Jembe FM Glory Kiwia amesema,kupitia mafunzo hayo yamemsaidia kufahamu shughuli zinazofanywa na mfuko huo  ikiwemo kuboresha mawasiliano kwa wananchi.

“Kupitia kalamu zetu tunaenda kuandika habari ambazo zitakuwa na tija na ubora kwa wananchi kwa kuelezea kwa usahihi shughuli na miradi inayotekelezwa na mfuko huo yenye kunufaisha jamii,”amesema Kiwia.

Mwenyekiti wa MPC Edwin Soko(aliyesima),akichangia mada katika mafunzo yaliotolewa na mfuko huo kwa Wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari Mkoa wa Mwanza,yaliofanyika wilayani Ilemela mkoani humo

Naye Mhariri wa Yohoma  Online TV  Silas Simon amesema,mafunzo hayo yamempa uwanja mpana wa kufahamu shughuli za mfuko huo na kwa namna gani anaenda kuelimisha jamii  kile ambacho UCSAF inafanya.

“Sehemu ambayo inakuza uchumi  ni mawasiliano  na kama yatakuwa na changamoto hakiwezi  kufanyika chochote cha kuleta maendeleo kwa Taifa,hivyo nitaenda kuelimisha jamii namna UCSAF inavyoboresha na kuendelea kutatua changamoto ya mawasiliano hapa nchini,”amesema Simon.