April 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Uchomaji misitu unaathari mazingira

Na Albano Midelo,TimesMajira online

TATIZO la uchomaji moto hovyo misitu ya hifadhi na maeneo yaliohifadhiwa kisheria linaleta athari za kimazingira katika maeneo mbalimbali nchini.

Kila mwaka majira ya kiangazi kuna matukio ya uchomaji moto hovyo misitu na mapori yanayosababisha hasara kubwa kiuchumi lakini pia kuathiri viumbehai wanaoishi katika maeneo hayo.

Kwa mfano kumekuwa na matukio ya uchomaji moto hovyo unafanyika katika Msitu wa Serikali wa SAO HILL wenye urefu wa kilometa 60 uliopo Mafinga Wilaya ya Mufindi Mkoa wa Iringa.

Msitu huo unapoteketezwa na moto unaleta athari kubwa kimazingira kwa sababu SAO HILL ni miongoni mwa chanzo cha mto Ruaha Mkuu ambao ni muhimu kwa viumbehai na uchumi wa Tanzania.

Wataalam wa mazingira wanaonya kuwa msitu wa SAO HILL ukiteketea wote kwa moto unaweza kusababisha hasara kubwa kwa serikali kwa kuwa gharama kubwa ilitumika na serikali kuanzisha msitu huo.

Msitu wa SAO HILL ulianzishwa katika kipindi cha awamu ya kwanza cha hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere ambapo serikali ilikopa Benki ya Dunia miaka ya 60 mamilioni ya dola za Marekani kwa ajili ya kuanzisha msitu huo.

Utafiti unaonesha kuwa Msitu wa SAO HILL ni moja ya mapafu ya Tanzania na endapo chanzo hicho kitaharibiwa kinaweza kusababisha chanzo cha maji cha mto Ruaha kilichopo katika msitu huo kuathirika hivyo Tanzania inaweza kupata athari kubwa za kimazinigira.

Ukiachia msitu wa SAO HILL,uchomaji misitu hovyo pia unaofanyika karibu kila mwaka katika Msitu wa Serikali wa Matogoro uliopo katika Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma hali inayoleta athari za kimazingira kwa kuwa msitu huo ni chanzo cha mito muhimu mitatu mikubwa.

Mito hiyo ni Ruvuma ambao unamwaga maji yake Bahari ya Hindi,Mto Luhira ambao ndiyo chanzo cha mto Ruhuhu unamwaga maji yake Ziwa Nyasa na Mto Luwegu ambao unachangia asilimia 19 ya maji katika Mto Rufiji ambao unaingia Bahari ya Hindi.

Mto Luhira ndiyo chanzo muhimu cha maji ambacho kinategemewa na Mamlaka ya Maji safi na Maji Taka Songea (SOUWASA) kwa ajili ya kusambaza maji katika Mji wa Songea.

Afisa Maliasili wa Mkoa wa Ruvuma Africanus Challe anasema Moto katika msitu wa Matogoro unateketeza eneo kubwa ambapo watumishi wa msitu huo kila mwaka wanafanya jitihada za kukabiliana na athari za uchomaji moto ikiwemo kutoa elimu kwa jamii kuhusu madhara ya moto kimazingira.

Challe anatoa rai kwa wananchi wanaozunguka msitu huo na kwa wadau wa mazingira wote kushirikiana na hifadhi ya misitu hiyo kukabiliana na matukio ya moto katika milima hiyo ili kuzuia uharibifu wa mazingira unaosababishwa na uchomaji wa moto kwenye msitu huo.

Anasema kutokana na uchomaji moto unaoendelea kufanywa ofisi ya hifadhi ya mlima Matogoro imefanya mazungumzo na mabonde ya maji ya ziwa Nyasa na bonde la maji ka mto Ruvuma ili kusaidiana kupanda miti ya asili katika maeneo yote ambayo yamevunwa miti na yalioungua ambapo mabonde yamechangia katika mradi wa miti.

Anasema Idara yake imechukua hatua mbalimbali za kulinda na kuhifadhi Msitu wa Serikali wa Matogoro na kuzuia uchomaji moto hovyo ambapo mwaka huu hadi sasa hakuna matukio ya moto kwenye msitu huo.

Afisa Maliasili huyo wa Mkoa wa Ruvuma anasema matukio ya uchomaji moto hovyo pia yamekuwa tishio katika Pori la Akiba la Wanyama la Liparamba Wilaya ya Nyasa na kuathiri hifadhi hiyo iliyopo mpakani na nchi Tanzania na nchi ya Msumbiji.

Anavitaja vijiji vilivyo kando kando mwa hifadhi ya Liparamba vinavyojihusisha na uchomaji moto hovyo ni Mitomoni, Mipotopoto, Mseto,Liparamba,Mpepai,Maleta,Mtua, Changarawe na Ndondo.

James Mbele Mkazi wa Kijiji cha Mitomoni anasema katika kijiji hicho kila mwaka wakulima wanasafisha mashamba yao kwa kuchoma moto badala ya kutumia njia nyingine mbadala ambazo haziwezi kuleta madhara kimazingira.

Mbele anatoa malalamiko yake kwa watendaji wa vijiji kushindwa kuwachukulia hatua wanaochoma moto hovyo ambapo amesema tangu alipofika katika Kijiji hicho mwaka 2002 hajawahi kuona mtu yeyote aliyechoma moto amechukuliwa hatua za kisheria.

Daudi Hyera ambaye ni Mwalimu katika shule ya msingi Mpepai anabainisha kuwa uchomaji moto unafanyika kutokana na wananchi wengi kuwinda wanyama hivyo wanachoma moto ili kutafuta urahisi wa kuwapata.

Sababu nyingine anaitaja kuwa ni watu wanaosafiri kwa miguu kupitia hifadhi ya Liparamba yenye msitu mnene na nyasi ndefu huamua kuchoma moto ili njia iwe wazi kwa kuhofia kukamatwa na wanyama wakali.
Mwenyekiti Mstaafu wa Kitongoji cha Makanga,Said Paulo anazitaja sababu za uchomaji moto hovyo misitu ni watu wanaochoma mkaa na wavutaji wa sigara au tumbaku.

Lazaro Joseph Mwenyekiti Mwanzilishi wa Kijiji cha Mtuha anasema wakati yupo madarakani alifanya jitihada kubwa za kutumia sheria ndogo ndogo ili kukabiliana na uchomaji moto hali iliyosababisha tatizo hilo kupungua.

“Baada ya kujiuzuru mwaka 1979 wenzangu waliofuatia walilegeza kamba ndipo fujo hiyo ya uchomaji moto iliendelea na hivi sasa tatizo la uchomaji moto limeongezeka’’anasema.

Uchunguzi umebaini kuwa misitu ya hifadhi na mapori huchomwa moto hovyo nyakati za kiangazi na hivyo kusababisha uharibifu mkubwa wa mazingira na upotevu wa bayoanuwai nyingi ya misitu.

Kulingana na utafiti,mikoa yote nchini yenye misitu aina ya miyombo, ina matukio mengi ya moto.Mikoa hiyo ni Rukwa, Mbeya, Tabora, Kigoma, Ruvuma, Lindi, Mtwara, Morogoro na Pwani.