Na Mwandishi Wetu,TimesMajira,Dar
WATANZANIA wamehamasishwa kupenda na kushiriki katika utalii wa ndani kwa kupanda Mlima Kilimanjaro na kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii hapa nchini.
Wito huo umetolewa jijini Dar-es-Salaam Septemba 10,2026 wakati wa uzinduzi wa kampeni ya Twenzetu Kileleni Msimu wa Tano, iliyoandaliwa na Kampuni ya Zara Tanzania Adventures.

Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa uzinduzi huo,Mkurugenzi wa Zara Tanzania Adventures, Zainab Ansell amesema,msimu huo utaenda sambamba na maadhimisho ya miaka 65 ya Uhuru wa Tanganyika, ambapo zaidi ya watu 200 wanatarajiwa kupanda Mlima Kilimanjaro.
Amesema vijana watakaowaunga mkono washiriki hao watafanya idadi ya watu watakaohusika katika kampeni hiyo kufikia zaidi ya 400.
“Kampeni hii inalenga kuwafanya Watanzania kutambua na kuthamini vivutio vya utalii vilivyopo hapa nchini,kwani wageni kutoka nje ya nchi wamekuwa wakifika kwa wingi kupanda Mlima Kilimanjaro,”amesema Ansell.
Amesema kabla ya kuanza safari ya kupanda mlima,washiriki watashirikishwa katika shughuli za uhifadhi wa mazingira ikiwemo upandaji miti, kwa lengo la kuhakikisha Mlima Kilimanjaro unaendelea kuwa rasilimali salama kwa vizazi vijavyo.
Ansell amesema,Watanzania ambao hawataweza kupanda mlima watapata fursa ya kuungana na wenzao katika safari za kutembelea maeneo mengine ya utalii yakiwemo Hifadhi za Taifa za Serengeti, Lake Manyara na Ngorongoro.
Amesema hatua hiyo itawapa wananchi fursa ya kujionea vivutio mbalimbali vya utalii kwa gharama nafuu, huku Zara Tanzania Adventures ikiendelea kushirikiana na jamii kupitia miradi mbalimbali ikiwemo kusaidia elimu na upandaji miti.
“Nawaomba Watanzania kutumia mwezi Desemba kutembelea Mlima Kilimanjaro na Serengeti ili kujionea utajiri wa utalii uliopo hapa nchini,”amesema.
Ofisa Masoko wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Albert Mboto amesema, juhudi zinazofanywa na Zara Tanzania Adventures zina mchango katika kuendeleza utalii wa ndani na kuunga mkono jitihada za Serikali za kukuza sekta hiyo hivyo wadau wanapaswa kutumia fursa hiyo kuhamasisha wananchi kutembelea vivutio vya utalii.

Kwa upande wake, Peter Mwambuga kutoka Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) amesema,huduma za mawasiliano zimeboreshwa katika eneo la Mlima Kilimanjaro ikiwemo uwezo wa mawasiliano kuanzia Lango la Marangu hadi kileleni ambayo yatasaidia washiriki kupata huduma za mawasiliano wakati wa safari na kurahisisha mawasiliano wanapokuwa mlimani.
Naye mwakilishi wa Chuo cha Taifa cha Utalii, Mary Maduhu amesema,kampeni hiyo ni fursa muhimu kwa wanafunzi na wafanyakazi kupata uzoefu wa moja kwa moja katika utalii wa milimani, uhifadhi wa mazingira na usimamizi wa urithi wa Taifa.

More Stories
Malisa aagiza watumishi kutatua kero za wananchi
QNET yaimarisha uongozi,Tanzania yawekwa kipaumbele
Tuzo za Wafugaji kuongeza tija ya Mifugo