Na Mwandishi Wetu,TimesMajira
WAFUGAJI nchini wanatarajiwa kuongeza tija na uzalishaji wa maziwa kupitia Mradi wa Tuzo Shindani za Watoa Huduma kwa Ajili ya Tasnia Himilivu ya Maziwa, unaolenga kuhamasisha matumizi ya mbinu bora za ufugaji, malisho bora na huduma zenye tija.
Mradi huo unaotekelezwa katika mikoa ya Iringa, Njombe, Mbeya na Morogoro, unalenga kuongeza uzalishaji wa maziwa, kipato cha wafugaji na kuboresha huduma zinazotolewa katika tasnia hiyo.
Akizindua mradi huo unaofadhiliwa na Heifer Intenational,Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Ng’wasi Kamani, amesema tuzo hizo ni sehemu ya jitihada za kuongeza tija katika ufugaji na uzalishaji wa maziwa kwa kuwahamasisha wafugaji kutumia teknolojia na mbinu bora za ufugaji.

Amesema Serikali itaendelea kutoa elimu kwa wafugaji kuhusu matumizi ya mbegu bora za malisho, uzalishaji wa malisho ya kutosha na matumizi ya teknolojia zinazoweza kuongeza uzalishaji wa mifugo.
Kamani amesema changamoto ya uzalishaji mdogo wa maziwa nchini inahitaji ushirikiano wa Serikali, wafugaji na wadau wa maendeleo ili kubadili hali hiyo na kuwawezesha wafugaji kuongeza kipato.

Amesema Serikali itaendelea kushirikiana na wadau kuhakikisha mradi huo unatekelezwa kwa ufanisi na unafikia malengo ya kuimarisha tasnia ya maziwa nchini.
Kwa upande wake, Msajili wa Bodi ya Maziwa, George Msaja, amesema mradi huo umeanzishwa kwa lengo la kuongeza uzalishaji na masoko ya maziwa, sambamba na kuboresha huduma kwa wafugaji.
Amesema unafadhiliwa na mashirika mbalimbali na unalenga kuwawezesha wafugaji kupata huduma bora zitakazowasaidia kuongeza uzalishaji na kupata masoko ya uhakika kwa maziwa yao.

Naye Mkurugenzi Mkazi wa Heifer International, Mark Tsoxo, amesema kaya nyingi nchini zinategemea tasnia ya maziwa, lakini uzalishaji bado ni mdogo, jambo lililosababisha kuanzishwa kwa mfumo wa tuzo unaolenga kuchochea matokeo katika sekta hiyo.
Amesema Heifer International imeanzisha mfumo wa kulipa kwa matokeo kupitia mradi huo, ili kuleta utaalamu katika utoaji wa huduma na kuhakikisha changamoto zinazowakabili wafugaji zinapatiwa ufumbuzi wa vitendo.

Muwasilishaji wa Mradi kutoka Heifer International, Edna Lusuva, amesema mahitaji ya maziwa nchini ni takribani lita bilioni 13 kwa mwaka, wakati uzalishaji uliopo ni lita bilioni 3.1, hali inayoonyesha pengo kubwa linalohitaji juhudi za makusudi.
Amesema moja ya sababu za uzalishaji kuwa mdogo ni wafugaji wengi kutumia ng’ombe wenye uwezo mdogo wa kutoa maziwa na kutotumia malisho bora.
Lusuva amesema tuzo hizo zitawahamasisha wafugaji kuongeza uzalishaji wa malisho bora na kutumia mbinu bora za ufugaji, hatua itakayosaidia kuongeza uzalishaji wa maziwa na kipato.
Amesema malengo makuu ya tuzo hizo ni kuongeza uzalishaji wa maziwa, kuimarisha uhusiano kati ya watoa huduma na wafugaji pamoja na kuongeza kipato cha wafugaji wadogo.
Katika hatua nyingine, Serikali imewataka wafugaji wanaofuga katika maeneo ya mabondeni kuchukua tahadhari na kuhamishia mifugo yao maeneo salama kutokana na uwezekano wa mvua za El Niño kusababisha mafuriko.
Kamani amesema wafugaji wanapaswa kuchukua hatua mapema badala ya kusubiri madhara yatokee, huku akisisitiza umuhimu wa maandalizi ya malisho na maeneo salama kwa mifugo.

Kwa upande wake, NBC ilieleza kuwa wafugaji watapata fursa za kupata mitaji ya kuendeleza shughuli zao, huku wakihimizwa kutumia mikopo hiyo kuwekeza katika uzalishaji.
Mwenyekiti wa Chama cha Wazalishaji Maziwa, Hamisi Mzee, amesema wafugaji wamepokea maelekezo yaliyotolewa na Serikali na wadau na watahakikisha wanayafanyia kazi ili kuongeza uzalishaji wa maziwa.
Naye Anna Almas mzalishaji maziwa kutoka Mvomero amesema wadau wa tasnia hiyo wanapaswa kutumia mradi huo kuboresha uzalishaji, malisho na huduma kwa wafugaji ili kuifanya tasnia ya maziwa kuwa na tija zaidi.

More Stories
Kigoma yatoa tenda zaidi ya Milioni 500
TMDA yakamata dawa zisizosajiliwa JNIA
Rashal yaharakisha Ujenzi wa Bomba la Gesi Kisemvule Mbagala