Na Mwandishi Wetu, Mwanza
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO),Lazaro Twange, amewataka wanasheria wa shirika kuendelea kusimamia maadili ya taaluma, kutoa ushauri wa kisheria kwa wakati na kulinda maslahi ya shirika ili kuimarisha utendaji na kuhakikisha TANESCO inaendelea kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.
Twange ameyasema hayo wakati akifungua Jukwaa la Wanasheria wa TANESCO lililoanza Julai 28, 2026 jijini Mwanza, likiwakutanisha wanasheria kutoka Makao Makuu, Ofisi za Kanda na Kampuni Tanzu za TANESCO kwa lengo la kujengeana uwezo na kubadilishana uzoefu kuhusu masuala ya kisheria yanayohusu utendaji wa shirika.
Akizungumza katika ufunguzi wa jukwaa hilo, Twange amewapongeza wanasheria hao kwa mchango wao katika kulinda maslahi ya shirika na kuhakikisha shughuli zake zinafanyika kwa kuzingatia sheria na taratibu.

“Nawapongeza kwa kazi nzuri mnayoendelea kuifanya. Ushauri wa kisheria unaotolewa kwa wakati umekuwa ukisaidia TANESCO kufanya maamuzi sahihi na kuepusha migogoro ambayo ingeweza kuzuilika mapema,” amesema Twange.
Amewasisitiza kuendelea kuzingatia maadili ya taaluma, kutunza siri za kazi na kutoa ushauri wa kitaalamu unaolinda maslahi ya shirika.

“Kila mmoja wetu ana wajibu wa kulinda taasisi. Kwa upande wa wanasheria, hilo linaanza na kuzingatia maadili ya taaluma, kutunza siri za kazi na kuhakikisha kila ushauri unaotolewa unalinda maslahi ya TANESCO na kuimarisha utendaji wake,” amesema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Huduma za Sheria wa TANESCO, Wakili Sundi Mahalu, amesema idara hiyo itaendelea kusimamia utekelezaji wa sheria, kanuni na miongozo mbalimbali ili kuhakikisha shughuli za shirika zinaendelea kufanyika kwa kuzingatia misingi ya utawala bora na sheria.

“Jukwaa hili linatupa nafasi ya kujifunza, kubadilishana uzoefu na kuimarisha uwezo wetu wa kitaaluma ili tuendelee kutoa huduma bora za kisheria zinazochangia mafanikio ya TANESCO,” amesema Wakili Mahalu.
Jukwaa la Wanasheria wa TANESCO linafanyika kwa siku tatu likiwa sehemu ya mkakati wa shirika wa kuendelea kuimarisha uwezo wa wataalamu wake wa sheria, hatua inayochangia ufanisi wa utendaji, usimamizi bora wa masuala ya kisheria na ulinzi wa maslahi ya shirika.

More Stories
Mwanasheria Mkuu wa Serikali ashiriki uzinduzi wa boti mpya za doria
Mchange ahoji Dkt.Nchimbi anajua madhara ya kauli zake
RC akabidhi magari matatu kwa Katibu Tawala