October 3, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Itunda: Vikundi 170 vyafaidika zabuni za asilimia 30

Na Mwandishi Wetu, TimesmajiraOnline, Mbeya

SERIKALI mkoani Mbeya imesema utekelezaji wa agizo la Rais Samia
la kutenga asilimia 30 ya zabuni kwa ajili ya vijana umeanza kuleta matokeo, huku Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya ikiwa tayari imenufaisha zaidi ya vikundi 170.

Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Solomon Itunda, amesema hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha vijana wanapata fursa za kiuchumi kupitia zabuni zinazotolewa na Halmashauri.

Amesema Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya tayari imetekeleza utaratibu huo, huku zaidi ya vikundi 170 vya vijana vikinufaika, wakati Halmashauri ya Jiji la Mbeya ikiwa imefikia vikundi 211.

Itunda ameyasema hayo Oktoba 2, 2026, wakati akifungua Kongamano la Vijana la mwaka 2026 lililofanyika Mbeya na kujadili fursa mbalimbali za kiuchumi kwa vijana, elimu, afya ya akili na masuala mengine muhimu.

Kongamano hilo limewakutanisha viongozi kutoka taasisi za Serikali, Jeshi la Polisi pamoja na taasisi za kifedha, waliotoa elimu na maelekezo kuhusu fursa zinazopatikana kwa vijana.

“Maana yake ni kwamba Mheshimiwa Rais Samia amedhamiria kwa dhati kuhakikisha vijana wa Mbeya wananufaika na fursa za Serikali katika maeneo yetu na Taifa kwa ujumla. Kwa niaba ya wananchi wa Mbeya, naomba nimshukuru Mheshimiwa Rais Samia,” amesema Itunda.

Aidha, Itunda amesema Serikali imeendelea kutekeleza mipango mbalimbali inayolenga kuwawezesha vijana, akitaja ongezeko la mikopo ya elimu ya juu na upatikanaji wake kwa wakati.

Amesema hatua nyingine ni kuboresha miundombinu ya elimu, ikiwamo shule za sekondari za bweni, shule kongwe, vyuo vikuu, maabara na ofisi za walimu, akieleza kuwa uwekezaji huo unagusa moja kwa moja maisha na mustakabali wa vijana.

Hata hivyo, Itunda amewataka vijana kutumia fursa zinazopatikana na kuchukua hatua zaidi katika kujikwamua kiuchumi badala ya kuendelea kulalamikia changamoto.

“Wakati wa kulalamika umekwisha. Kilichobaki ni kuchukua hatua zaidi za kujikwamua kimaisha kwa kutumia fursa zilizopo,” amesema.

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Utengule Usongwe na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, Aida Haule, amewataka vijana kuwa wazalendo na kutumia fursa zinazotolewa na Serikali kwa manufaa yao na taifa.

“Mheshimiwa Rais Samia anatamani kuona kizazi hiki na kijacho kinapata fursa za Serikali. Jukwaa hili la vijana tutumie fursa za kiuchumi kuhakikisha mnajikomboa kimaisha kwa kutumia fursa zilizopo,” amesema Haule.

Naye Afisa Tawala wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, Devotha Chacha, amewataka vijana na wanafunzi kukabiliana na changamoto wanazokutana nazo katika safari ya kufikia ndoto zao.

Chacha pia amewataka vijana ambao si wanafunzi kutumia simu zao na teknolojia nyingine za kidijitali kama fursa za kujifunza, kujiajiri na kujenga shughuli za kiuchumi.