May 8, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Tume ya Madini yavuka lengo utoaji leseni

Na Joyce Kasiki, Timesmajira online,Dodoma

KAIMU Katibu Mtendaji Mkuu wa Tume ya Madini Mhandisi Ramadhan Lwamo  amesema,katika mwaka wa fedha 2022/23,imefanikiwa kutoa jumla ya leseni 9,642 kati ya leseni 9,174 zilizopangwa kutolewa katika kipindi hicho.

 Akizungumza na waandishi wa Habari jijini hapa kuhusu utekelezaji wa taasisi hiyo kwa mwaka wa fedha wa 2023/24,Mhandisi Lwamo amesema,hatua hiyo  ni kuimarisha uwekezaji katika sekta ya hiyo nchini.

Aidha amesema , leseni hizo zilijumuisha leseni za uchimbaji mkubwa, uchimbaji wa kati, uchimbaji mdogo, biashara ya madini pamoja na uchenjuaji wa madini,

“Kati ya leseni zilizotolewa leseni 6,511 sawa na asilimia 70.97 zimetolewa kwa wachimbaji wadogo,hiyo inadhihirisha azma ya serikali ya awamu ya sita katika kuwaendeleza wachimbaji wadogo na kuongeza mchango wao katika sekta ya madini.”amesema Mhandisi Lwamo na kuongeza kuwa

“Muelekeo wa sekta ya madini unalenga katika kuhakikisha mchango wa sekta ya hii katika Pato la Taifa unafikia asilimia 10 au zaidi ifikapo mwaka 2025 kama inavyofafanuliwa katika dira ya maendeleo ya Taifa,ilani ya chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2020 pamoja na Mpango mkakati wa Tume ya madini wa mwaka 2019/20-2023/24,”

Aidha amesema,Tume ya madini kwa  kushirikiana na Mamlaka za Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) imefanikiwa kuanzisha jumla ya masoko ya madini 42 na vituo vidogo vya ununuzi wa madini 94 nchini.

Kuhusu  uanzishwaji wa masoko hayo  Mtendaji huyo amesema ulianza rasmi tarehe 17 March 2019 kwa lengo la kuimarisha udhibiti wa biashara ya madini nchini ili kuongeza mapato yatokanayo na rasilimali madini kwa Serikali.

“Katika  mwaka wa fedha 2022/2023 masoko na vituo vya ununuzi wa madini vilichangia jumla ya shilingi milioni 157.428 kama mrahaba na ada ya ukaguzi wa madini nchini sawa na asilimia 23.22 ya makusanyo yote yaliyokusanywa na Tume kwa mwaka husika.”

Akielezea kuhusu majukumu ya Tume.hiyo Mhandisi Lwamo amesema,Tume ya Madini ni Taasisi iliyo chini ya Wizara ya madini ambayo iliundwa na sheria ya madini sura ya 123 na kutangazwa kwenye gazeti la Serikali Na.27,na ilianza kutekeleza majukumu yake rasmi tarehe 17 aprili 2018.

Kwa.mujibu wa kiongozi huyo,lengo kuu la kuundwa kwa Tume ni kuboresha usimamizi na Udhibiti katika ukaguzi wa uzalishaji na biashara ya madini kwa kuhakikisha sheria,kanuni na taratibu zote zinazoongoza shughuli za madini zinafuatwa ipasavyo ili kuongeza pato la Taifa.

Hata hivyo amesema,majukumu ya Tume ya madini yamefafanuliwa katika sheria ya madini sura ya 123 kifungu cha 22 ambayo yanalenga kusimamia shughuli zote zinazohusiana na madini nchini.