Na Judith Ferdinand, Timesmajira Online- Mwanza
SERIKALI imefanya uwekezaji wa zaidi ya shilingi trilioni moja ili kuimarisha usafiri kwa njia ya maji kwa kununua meli mpya, kukarabati zilizopo na kuboresha miundombinu yake.
Miundombinu hiyo ndio inayojenga Ushoroba wa Kati ambao ni kiungo muhimu si tu kwa usafirishaji wa shehena ya mizigo ndani ya nchi bali pia kwa nchi za jirani ambazo hazipakani na bahari.
Hayo yameelezwa Machi 22, 2026 mkoani mwanza, na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo ambaye ni Msemaji Mkuu wa Serikali,Gerson Msigwa,wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya utendaji wa serikali katika sekta ya uchukuzi.
Msigwa amesema,wakati Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alipoingia madarakani, ujenzi wa meli ya MV.Mwanza ulikuwa asilimia 40 huku kiasi cha shilingi bilioni 36 pekee ndio kilikuwa kimelipwa,lakini kwa sasa mradi umekamilika ambao umegharimu jumla ya shilingi bilioni 120.
Amesema,Serikali imekamilisha ukarabati wa meli ya MV.Umoja katika Ziwa Victoria kwa gharama ya shilingi bilioni 22.9.Mradi huo unatarajiwa kuwa kiungo muhimu kwa mizigo inayopitia Ushoroba wa Kati kwa njia ya reli kuelekea Uganda na Sudani Kusini.
Pia amesema,Serikali inaendelea na ukarabati wa meli ya MT.Ukerewe katika Ziwa Victoria kwa gharama ya shilingi bilioni 7.5, hadi sasa utekelezaji wake umefikia asilimia 72,ambayo ni tegemeo katika shughuli za uokozi,kupandisha na kushusha meli zinazojengwa au kufanyiwa matengenezo kwenye chelezo.
Aidha Msigwa,amesema Serikali inaendelea na ujenzi wa meli mpya ya mizigo itakayotoa huduma ndani ya ziwa Victoria, ikiwa na uwezo wa kubeba tani 3,000 za mizigo kwa gharama ya zaidi ya shilingi bilioni 145.4,ukarabati wa meli ya MV.Liemba yenye uwezo wa kubeba abiria 600 na tani 200 za mizigo kwa gharama ya shilingi bilioni 32.9 na ujenzi umefikia asilimia 55,unatarajiwa kukamilika Julai 2026.
Mradi wa meli mpya ya mizigo itakayotoa huduma Ziwa Tanganyika utagharimu zaidi ya shilingi bilioni 158.27,ikikamilika itakuwa na uwezo wa kubeba tani 3,500 za mizigo, kupakia malori marefu 25 au mabehewa 25 ya reli ya kisasa na magari madogo 65.
Vilevile amesema mradi mwingine ni wa ujenzi wa meli nne kubwa za mizigo Bandari ya Karema,umefikia asilimia 95 na unatarajiwa kukamilika Julai, 2026.
Sanjari na hayo amesema,Serikali inatekeleza mradi wa usanifu na ujenzi wa gati jipya pamoja na mfumo wa ‘conveyor belt’katika bandari ya Kisiwa Mgao kwa gharama ya shilingi bilioni 434.53.Hadi Februari 2026, shilingi bilioni 128.20 zimetumika na utekelezaji wake umefikia asilimia 33.

More Stories
NMB ilivyosaidia Serikali kukusanya zaidi ya Sh trilioni 9.8
Serikali yaongeza nguvu kwa wachimbaji wadogo,yasisitiza usalama Migodini
REA imeleta mageuzi sekta ya nishati