Na.Mwandishi wetu,Timesmajira
Chama cha Mawakili wa Serikali Tanzania (TPBA) kinatarajia kuzindua rasmi kitabu maalum kinachoitwa “Falsafa ya Sheria ya Mama Samia” (Mama Samia Doctrine of Law), ambacho kimeandaliwa kwa lengo la kuandika na kuhifadhi historia ya mageuzi mbalimbali yaliyofanyika nchini chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Uzinduzi huo unatarajia.kufanyika Juni 12, 2026 katika Ukumbi Mpya wa Maktaba wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba.
Kwa mujibu wa TPBA, kitabu hicho ni matokeo ya utafiti wa kina uliohusisha uchambuzi wa takwimu, nyaraka rasmi za serikali na maoni ya wataalamu mbalimbali kuhusu mabadiliko yaliyofanyika katika sekta tofauti za maendeleo nchini.
Kitabu hicho kinaangazia kwa undani mageuzi ya sheria na utoaji wa haki, ukuaji wa uchumi, uwekezaji, diplomasia, utawala bora, matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA), elimu, afya pamoja na maendeleo ya kijamii yaliyotekelezwa katika kipindi cha uongozi wa Rais Samia.
Aidha, kitabu hicho kinaeleza namna mageuzi hayo yanavyohusiana na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 hadi 2050, huku kikionesha mchango wa sheria, sera na uongozi katika kujenga msingi wa maendeleo endelevu ya Tanzania ya baadaye.
TPBA imeeleza kuwa kabla ya kuchapishwa, kitabu hicho kilipitia mchakato wa uhakiki wa kitaalamu uliofanywa na maprofesa, watafiti na wataalamu mbalimbali waliolenga kuhakikisha usahihi wa maudhui, takwimu na mchango wake katika maendeleo ya taifa.
Uzinduzi huo pia unatarajiwa kuhudhuriwa na viongozi wa serikali, wanataaluma, watafiti, wanafunzi wa sheria, mawakili pamoja na wadau mbalimbali wa maendeleo.
Taarifa hiyo imesema mlezi wa TPBA na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Hamza Johari, anatarajiwa kushiriki katika hafla hiyo ambayo waandaaji wameielezea kuwa ni fursa muhimu ya kutafakari mchango wa sheria katika maendeleo ya taifa na kuangalia mwelekeo wa Tanzania kuelekea Dira ya Maendeleo ya mwaka 2050.
Kaulimbiu ya kitabu hicho ni “Falsafa ya Sheria ya Mama Samia: Mageuzi, Uongozi na Dira ya Tanzania ya Kesho,” ikilenga kuonyesha nafasi ya sheria na uongozi katika kuharakisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini.
TPBA imewataka Watanzania wote kujitokeza kushiriki katika uzinduzi huo wa kihistoria ili kujionea maudhui ya kitabu hicho na kujifunza kuhusu safari ya mageuzi ya Tanzania katika kipindi cha uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan.

More Stories
Salome:Ushirikiano wa wadau ni muhimu kufikia lengo la Nishati Safi ya Kupikia
Wazalishaji teknolojia nishati safi watakiwa kufuata viwango
Mgawanyo wa hisa NMB wafungua mlango kwa wawekezaji wapya