May 15, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TPA yafafanua mikataba ya watumishi kuhusu kuhamia DP World

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

MAMLAKA ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imetoa ufafanuzi kuhusu hali ya ajira kwa watumishi wa bandari ya Dar es Salaam.

Katika taarifa iliyotolewa mapema leo imesema kuwa mnamo Jumatano tarehe 20 Machi, 2024 TPA ilitoa taarifa kwa watumishi wake kuhusu mabadiliko ya uendeshaji wa Bandari ya Dar es Salaam, Gati namba sifuri (RoRo) hadi Gati namba saba.

Mabadiliko hayo yanatokana na mkataba kati ya TPA na Kampuni ya DP World ya Dubai kuhusu uendeshaji na endelezaji wa gati 0 – 7 za Bandari ya Dar es Salaam kwa kipindi cha miaka thelathini (30) kuanzia tarehe 22 Oktoba 2023.

Taarifa hiyo inasema kutokana na mabadiliko ya usimamizi na endeshaji wa maeneo tajwa, watumishi wa Bandari ya Dar es Salaam walitakiwa kuchagua kusitisha mkataba wa ajira na TPA au kuajiriwa na DP World.

Menejimenti ya TPA ilitoa taarifa hiyo kwa watumishi baada ya kukamilisha programu maalum ya kuwaelimisha na kutoa ufafanuzi wa kina na taarifa sahihi kuhusiana na mabadiliko tajwa kwa watumishi wake.

Aidha taarifa hiyo imeeleza kuwa watumishi watakaoridhia kujiunga na DPW kwa hiyari walielekezwa kuwasilisha taarifa zao (Notice) katika ofisi zilizopo ghorofa ya 32 katika Jengo la Makao Makuu ya TPA (One Stop Centre) kabla au ifikapo tarehe 29 Machi, 2024. Kwa wale hawatajiunga na DP World watabaki TPA kwa kuwa mamlaka itaendelea kuhitaji watumishi watakaotoa huduma katika bandari zake zinazoendelea kuboreshwa katika maeneo mbalimbali nchini.

“ Menejimenti ya TPA imeujulisha umma kwamba, taarifa inayosambaa ilitolewa kwa ajili ya watumishi na TPA ilifanya hivyo ili kukamilisha taratibu za kuhamisha huduma kwa DP World,

TPA inauhakikishia umma kwamba, itaendelea kuwathamini watumishi wake ambao ni rasilimali muhimu zaidi katika mamlaka na katika utekelezaji wa zoezi hili, maslahi ya pande zote husika yatazingatiwa kikamilifu kwa mujibu wa sheria za nchi yetu ” ilieleza taarifa hiyo