April 28, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TOSCI yawabana wauzaji holela wa mbegu



‎Na Israel Mwaisaka, Nkasi

‎Taasisi ya Udhibiti wa Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI) imefanya ukaguzi wa mbegu katika maduka ya pembejeo za kilimo wilayani Nkasi, mkoani Rukwa, na kupiga marufuku uuzaji wa mbegu katika maeneo ya minadani.

‎Zoezi hilo limeongozwa na maafisa wakaguzi kutoka (TOSCI), wakiongozwa na Frank Steven, kwa kushirikiana na maafisa kilimo wa wilaya Nkasi.

‎Ukaguzi huo umebaini kuwa jumla ya maduka 45 yamekaguliwa, huku baadhi ya wakulima wakigundulika kununua mbegu katika maeneo yasiyo rasmi badala ya maduka yaliyosajiliwa.



‎Akizungumza wakati wa ukaguzi huo, Afisa Kilimo wa Wilaya ya Nkasi, Emmanuel Gamasa, aliwataka wafanyabiashara kuzingatia sheria na taratibu za uuzaji wa pembejeo za kilimo.

‎“Ni muhimu kwa wauzaji wote wa pembejeo kufuata utaratibu uliowekwa na serikali. Uuzaji wa mbegu katika maeneo yasiyo rasmi unahatarisha ubora wa kilimo na unaweza kusababisha hasara kwa wakulima,” alisema Gamasa.

‎Aidha, aliwahimiza wakulima kuacha kununua mbegu katika maeneo yasiyo rasmi na badala yake wanunue katika maduka yaliyosajiliwa ili kupata mbegu bora na zenye uhakika wa mavuno.

‎Kwa mujibu wa TOSCI, matumizi ya mbegu bora ni hatua muhimu katika kuongeza uzalishaji wa mazao na kuinua uchumi wa mkulima mmoja mmoja pamoja na taifa kwa ujumla