April 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

THRDC yamuomba Rais Samia kuingilia kati mgogoro wa Wananchi Loliondo na watu wahifadhini

Na Penina Malundo,Timesmajira,Online

MTANDAO wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) umemuomba Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kutoa nafasi na kuwasikiliza wananchi wa vijiji vya Loliondo vilivyopo wilayani Ngorongoro wanaokabiliwa na mgogoro wa ardhi wa muda mrefu.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Mratibu kitaifa wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania ,(THRDC), Onesmo Olengurumwa alisema mgogoro huo umekuwa wa muda mrefu kati ya Wananchi, wahifadhi wa Mamlaka za Hifadhi na Wizara ya Maliasili ambao unadaiwa kuendelea kukua wilayani Ngorongoro na kuleta hofu kwa jamii.

Amesema THRDC inaamini kuwa Rais Samia akitoa nafasi ya kuwasikiliza wananchi hao huenda akawa Rais wa kwanza kupatia ufumbuzi wa kudumu migogoro ya ardhi na uhifadhi wilayani Ngorongoro.

“Tunamuomba Rais Samia awape nafasi na kuwasikiliza wananchi hawa wa Loliondo kusikia hoja zao na hatimaye azifanyie kazi ili kumaliza mgogoro huo wa muda mrefu, ” amesema Olengurumwa

Olengurumwa amesema wanaiomba pia Serikali kusitisha mpango wake wa kuchukua ardhi za vijiji hivyo badala yake ikae na wananchi hao na kutafuta suluhu itakayokubaliwa na pande zote.
“Uhamisho huo wa wananchi utakapofanywa ufanywe kwa mujibu wa sheria na taratibu za nchi na mikataba ya kimataifa,”amesema na kuongeza

“Tunapendekeza migogoro hii baina ya wananchi wa Ngorongoro, Loliondo na wahifadhi ufanyiwe usuluishi wa kudumu, tunapendekeza apatikane msuluhishi ambaye hana maslahi pande zote mbili au msuluhishi mkuu awe Rais Samia kwa kuwa yeye ana maslahi pande zote mbili ambapo kwa wananchi ni wapiga kura wake na wananchi wake, taasisi za Uhifadhi zipo chini yake,” amesema