April 19, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

THRDC kuendelea kuimarisha utetezi haki za binadamu mikoa ya kusini

Na Mwandishi wetu,timesmajira,online

MRATIBU Kitaifa wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Onesmo Olengurumwa amaliza ziara yake kwa kanda ya pwani ya kusini kwa mikoa ya Lindi, Mtwara, na Ruvuma kwa lengo la kuimarisha utetezi wa haki za binadamu katika mikoa hiyo.

Akizungumza katika ziara hiyo,Olengerumwa ameahidi kuzifanyia kazi changamoto mbalimbali zinazokwamisha shughuli za utetezi wa haki za binadamu katika mikoa hiyo.

“Mtandao kufahamu changamoto mbalimbali zinazowakabili wanachama wa kanda hiyo hivyo mnapaswa kuunda mikakati kadhaa ya kuwastawisha wanachama wenu katika kanda hii.”amesema

Amesema mtandao umejifunza maeneo ya kuboresha katika mashirikiano yake na wanachama wa kanda hiyo.”Wanachama wa Mtandao wa Kanda ya pwani ya kusini wamesifika kua na mahusiano mazuri sana na mamlaka husika katika maeneo yao ya kazi, pamoja na polisi, ustawi wa jamii, na hata mashirika mengine,”amesema na kuongeza

“Hii imewasaidia kutekeleza majukumu yao na kuifikia jamii husika kwa urahisi zaidi kwani Mashirika yamefanikiwa kuendesha programu mbali mbali za utoaji elimu kwa jamii na huduma za msaada wa sheria kwa mtu mmoja mmoja kupitia wasaidizi wa kisheria (Legal Aid Providers) katika masuala ya Elimu ya Sheria pamoja na elimu kupitia vipindi vya radio na kuwafikia jamii na kuelimisha,”amesema

Amesema pamoja na mafanikio makubwa ya mtandao kwa wanachama wake bado changamoto kadhaa zimekuwa zikiwakumba wanachama wa mtandao ikiwemo changamoto za kifedha, kwani kutokana na masuala ya UVIKO 19, ambapo fedha nyingi zinazotolewa na wahisani huelekea katika miradi mingine ya kupambana na janga la CORONA kubadili uelekeo,Taasisi nyingi kutokuwa na ofisi yenye nafasi kubwa ya kutosheleza wafanyakazi wote kwa shughuli za kitaasisi.

Changamoto nyingine ni kutokuwa na miradi endelevu inayoweza kusaidia mashirika kufanya shughuli kwa Muda mrefu, na kuweza kuisaidia jamii na matokeo yake kunakuwa na miradi ya muda mfupi ambayo haitatui matatizo kwa kiasi kinachotakiwa,Ugumu katika upatikanaji wa ‘charitable Status’ ambao ungeziwezesha taasisi kupata msamaha wa kodi mbali mbali na kuweza kujiendesha pamoja na mashirika yanayotetea haki za Watoto wa kike, kukumbwa na changamoto kubwa ya utoroshwaji wa watoto ambao hufanywa na wazazi pindi watoto wanaporudi nyumbani kwa likizo na kuozeshwa kwa lengo la kujipatia mali.