April 29, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Telack awataka wakazi wa Kilwa kuwa tayari kuwapokea watalii

Na.Penina Malundo, timesmajira

MKUU wa Mkoa wa Lindi, Zainab Telack amewataka wakazi wa wilaya ya Kilwa na Mkoa wa Lindi kuwa tayari kuwapokea watalii wanaotembelea Hifadhi ya Urithi wa Dunia ya Magofu ya Kilwa kisiwani na Songo Mnara na kutumia fursa hiyo kufanya biashara za bidhaa za utalii ili kuwaingizia kipato.

Zainab ameyasema hayo jana akiongea na waandishi wa habari ndani ya Hifadhi ya Urithi wa Dunia ya Magofu ya Kilwa kisiwani na Songo Mnara wakati wa mapokezi ya Meli ya Saba kuingia Hifadhini humo katika kipindi cha mwezi Februari ikiwa na idadi ya watalii 120 kutoka Mataifa mbalimbali Duniani.

Amesema mfululizo wa safari za Meli za watalii ndani ya Hifadhi hiyo ni kiashiria kwamba filamu ya Tanzania The Royal Tour iliyochezwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeleta matokeo chanya kwa Mkoa wa Lindi na Tanzania kwa ujumla.

Mkuu huyo wa Mkoa amesisitiza kuwa Hifadhi ya Urithi wa Dunia ya Magofu ya Kilwa kisiwani na Songo Mnara iliyo chini ya usimamizi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) inatarajia kupokea Meli nyingine zaidi za watalii Mwezi Machi na April hivyo wakazi wa Mkoa huo watumie vyema ujio wa Meli hizo.

Aidha ametumia fursa hiyo kuwaalika watu wote wenye bidhaa zinazopendwa na watalii na kuziuza wakati wa safari za wageni ndani ya Hifadhi hiyo huku alisisitiza kuwa TAWA imejenga jengo la kisasa na maalumu kwa ajili ya wafanyabiasha wa bidhaa za kitalii, hivyo walitumie jengo hilo ipasavyo.

Akibainisha sababu za watalii wengi kutembelea Hifadhi ya Urithi wa Dunia ya Magofu ya Kilwa kisiwani na Songo Mkuu wa Hifadhi hiyo Mercy Mbogelah amesema majengo ya kale yaliyojengwa zaidi ya miaka 1000 iliyopita kama vile msikiti mkubwa na mkongwe kuliko yote katika ukanda wa Pwani ya Afrika Mashariki na ngome ya Mreno ni vivutio vikubwa vya watalii vinavyowafanya watalii wengi kumiminika katika Hifadhi hiyo.

Amesema kutokana na historia hiyo kubwa ndani ya Hifadhi ya Kilwa kisiwani Mwaka 1981 Shirika la Kimataifa la UNESCO liliipa hadhi Hifadhi hiyo na kuwa Hifadhi ya Urithi wa utamaduni wa Dunia na baadae Mwaka 2023 kuwepa hadhi nyingine kuwa “Man and Biosphere Reserve”. Vigezo vyote hivi vimetajwa kuwa mojawapo ya sababu za watalii wengi kutoka nje kupenda kuitembelea.

Naye Afisa Utalii wa Hifadhi hiyo, Shindawangoni Rajabu amesema Hifadhi ya Urithi wa Dunia ya Magofu ya Kilwa kisiwani na Songo Mnara imekuwa ikipokea Meli kubwa za watalii na Mwaka huu wa 2024 imepokea Meli nyingi zikiwa na idadi kubwa ya watalii katika kipindi kifupi ikilinganishwa na miaka mingine yote na inatarajia kuendelea kupokea Meli nyingine zaidi za watalii kutoka Mataifa mbalimbali Duniani.

Amesema ongezeko la idadi ya Meli zenye idadi kubwa ya watalii ni kiashiria tosha kuwa Hifadhi hiyo inaendelea kivutio kizuri zaidi Duniani.