Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online, Dar es Salaam
JUKWAA la Wahariri Tanzania (TEF) imesema kuna matarajio mapya ya uhuru wa vyombo vya habari nchini kutokana na kauli ya Rais Sama Suluhu Hassan kuagiza baadhi ya vyombo vya habari kufunguliwa huku kukiwa na nafasi ya majadiliano kwa vingine.
Akizungumza wakati wa mdahalo uliofanyika jijini Dar es Salaam ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha siku ya vyombo wa habari Mei 03 uliolengwa matokeo ya Kauli ya Rais Samia ya Kufunguliwa kwa baadhi ya vyombo vya habari , Katibu wa Jukwaa hilo Neville Meena amesema hiyo ni nguvu ya kupiga hatua nyingine katika kudai uhuru wa habari na vyombo vya habari.
Meena amesema kauli hiyo imeonesha kuwa serikali inatoa nafasi za majadiliano na vyombo vya habari hivyo ni nafasi kwao kupigia kelele sheria kandamizi kwao.
“Kauli iliyotolewa na mheshimiwa Rais ni mwanzo bora na mzuri kwa vyombo vya habari imetuonesha njia ya kupita na kutupa matumiani ya ushirikiano na utayari wa serikali katika kutambua muhimili huu, hivyo huu ni mwanzo kwa taasisi mbalimbali za tasnia ya habari kuungana pamoja na kuweka mawazo sawa kwa ajili ya kuiendea serikali tukiwa na sauti moja.
“Hatua hii inatupa nafasi ya kufanyia kazi changamoto zinazoikabili tasnia ya habari,” amesema Meena.
Katika mdahalo hue pia wadau walijadili sababu za wamiliki wa vyombo vya habari kutokuwa na maslahi mapana ya waandishi wa habari ikiwemo kupata bima ya afya na kupata stahiki zao pindi wanapofukuzwa kazi au kampuni kufungwa.
Akijibu hoja hiyo kwa upande wa Wamiliki wa Vyombo vya habari, Deodatus Balile ambaye pia ni Kaimu Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri, amesema changamoto inayojitokeza ni waandishi kushindwa kuwa wabunifu na kuwajibika ipasavyo.
“Suala hili la maslahi limekuwa na ukakasi, kwani wamiliki wanalalamika kuwa waandishi hawawajibiki ipasavyo, huku Waandishi nao wakisema kuwa mazingira ya kazi yamekuwa ni magumu, hivyo imekuwa ni kurushiana mpira.
“Kitu kingine ni vyombo vya habari kukosa matangazo hali inayofanya kuwa ngumu kuingiza kipato na kuwalipa waandishi vizuri ,”amesema Balile.
Mjandala huo ulishirikisha wadau lkutoka taasisi mbalimbali ikiwamo Chama Cha wamiliki wa vyombo vya habari nchini (MOAT), Internews ,Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu na taasisi nyingine.
Aprili 6, mwaka huu Rais Samia aliiagiza Wizara ya Habari kuvifungulia vyombo vya habari vilivyokuwa vimefungiwa huku akisisitiza vyombo vya habari viachwe vifanye kazi yake, aidha Aprili 22, mwaka huu wakati akilihutubia Bunge kwenye sehemu ya hotuba yake alibainisha kuwa; “Maeneo mengine ni pamoja na kuendelea kulinda misingi ya demokrasia na uhuru wa watu pamoja na vyombo vya habari,” alisema Rais Samia.
More Stories
RC Mrindoko:Vyombo vya haki jinai shirikianeni kumaliza kesi kwa wakati
RC Katavi ataka huduma ya maji safi na salama iimarishwe kudhibiti Kipindupindu
Walengwa TASAF Korogwe TC watakiwa kuchangamkia fursa