April 23, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TCDC kuzindua kampeni kuimarisha Ushirika

Na Joyce Kasiki,Dodoma

MRAJISI na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), Dkt. Bendon Ndiege, ametangaza kufanyika kwa mkutano mkubwa wa wadau wa maendeleo ya ushirika pamoja na uzinduzi wa kampeni maalum ya kuimarisha uadilifu na uwajibikaji katika vyama vya ushirika nchini.


Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jijini Dodoma Aprili 22,2026 Dkt. Ndiege amesema mkutano huo unalenga kujadili hali ya sekta ya ushirika na kuweka mikakati madhubuti ya kukabiliana na changamoto zinazoikabili, hususan masuala ya uadilifu katika utekelezaji wa shughuli za vyama vya ushirika.


Amesema serikali imeandaa mkutano huo kama sehemu ya juhudi za kuimarisha uwajibikaji na kurejesha imani ya wanachama pamoja na wadau wengine katika vyama vya ushirika, ambavyo ni mhimili muhimu wa maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi.


“Lengo kuu ni kuimarisha ushirikiano wa wadau wote wa sekta ya ushirika katika kulinda maslahi ya wanaushirika na kuhakikisha kuwa vyama vya ushirika vinakuwa chombo imara cha maendeleo ya wananchi,” amesema Dkt. Ndiege.


Katika mkutano huo, TCDC inatarajia kuzindua rasmi kampeni yenye kaulimbiu isemayo “Linda Ushirika, Chagua Uadilifu”, inayokusudia kujenga msingi imara wa uwajibikaji, haki na utawala bora katika sekta ya ushirika.


Kwa mujibu wa Dkt. Ndiege, kampeni hiyo inalenga pia kuzikutanisha taasisi mbalimbali zinazohusika na usimamizi wa sekta hiyo ili kujenga uelewa wa pamoja utakaosaidia kuondoa changamoto za uaminifu na uwajibikaji.


Mkutano huo utafanyika Aprili 24, 2026 katika jiji la Dodoma, ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri wa Kilimo, Daniel Chongolo.
Washiriki wa mkutano huo watajumuisha viongozi na watendaji wa vyama vya ushirika, wadau kutoka taasisi za haki kama mahakama, TAKUKURU na Jeshi la Polisi, pamoja na wakuu wa mikoa, wilaya, wakurugenzi wa halmashauri na wabunge.
Aidha, watoa huduma mbalimbali wanaohudumia vyama vya ushirika pia wamealikwa kushiriki ili kuhakikisha utekelezaji wa kampeni hiyo unakuwa shirikishi na wenye tija kwa sekta nzima.


Dkt. Ndiege amesisitiza kuwa wadau wote walioalikwa wanatarajiwa kutoa maoni yao ili kuboresha kampeni hiyo na kuhakikisha inaleta matokeo chanya katika kuimarisha uadilifu na uwajibikaji katika vyama vya ushirika nchini.