January 11, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TBA yapewa siku 14 kutatua kero za wapangaji Ilala

Na Agnes Alcardo, Timesmajira Online, Dar

MKUU wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, ametoa siku 14 kwa uongozi wa Wakala wa Majengo Tanzania TBA, Mkoa wa Dar es Salaam, kukaa na wapangaji wake wa Ilala Kota, ili kutatua kero walizonazo na endapo watashindwa kuafikiana ziwasilishwe ngazi za juu ili ziweze kutatuliwa.

Agizo hilo, limetolewa Disemba 9, mwaka huu Jijini Dar es Salaam na Mkuu wa Wilaya hiyo, alipokutana na wakazi hao, wanaoishi kwenye nyumba ambazo zimeonekana kutokarabatiwa kwa muda mrefu, zilizopo katika Kata ya Mchikichini, zijulikanazo kwa jina la Ilala Kota.

Wakazi hao wameilalamikia TBA kuwalipisha tozo na kuongeza malipo ya kodi ya pango, bila kuzifanyia ukarabati nyumba hizo kwa kipindi Cha muda mrefu hadi sasa na kudaiwa kuwa, wakimtaka mpangaji kuhama pindi anapoomba kufanyiwa ukarabati kwenye nyumba anayoishi inapokuwa imeharibika.

Aidha, wengine wamelalamikia kunyang’anywa kwa vibanda ambavyo walivijenga kwa muda mrefu kwa ajili ya kuwaendeshea maisha yao kwa kipindi ambacho wamekuwa wakiishi hapo.

“Natoa muda wa siku 14 TBA, Mkae na Wawakilishi wa Wakazi hawa na mimi naongeza maafisa watatu wa Serikali, ambao watashiriki kwenye mazungumzo hayo na mtakachokubaliana kifikishwe mara moja sehemu husika, mtakapo kaa mzingatie falsafa ya Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan ya Maridhiano.

Pia, vibanda ambavyo tayari vilikuwa vimeshajengwa na wakazi hawa kwa ajili ya kujikimu kimaisha visibomolewe wala kuhamisha umiliki kwa kificho hadi hapo mtakapo kuwa mmekaa na kukubaliana, ingawa vibanda vipya visijengwe,” amesema Mpogolo.

Akiwasilisha changamoto walizonazo wakazi hao, Mwenyekiti wa Wakazi wa Ilala Kota, Charles Kapongo, mbele ya mkuu wa wilaya hiyo, kwa umoja wao amedai kuwa, wakazi hao wamekuwa wakikabiliwa na changamoto nyingi za kimiundombinu kwa muda mrefu bila ya kupatiwa ushirikiano na TBA.

Mmoja wa wakazi aliye hudhuria katika mkutano huo, Eltimus Msamba Mkazi ambaye inaelezwa ameishi kwenye nyumba hizo tangu mwaka 1956, amesema wamekuwa wakibeba jukumu la kukarabati wenyewe nyumba zao kutokana na mmiliki wa nyumba hizo, ambaye ni TBA kutofanya ukarabati pindi inapotolewa taarifa na badala yake kumtaka mpangaji kuhama.

“Mimi ni Mkazi wa hapa kwa muda mrefu na nyumba hizi wakati tunaingia zilikuwa na choo, maji, umeme. Lakini kama binadamu ilibidi niingize maji na umeme mwenyewe baada ya nyumba kubomoka kwani nilipowaambia kuwa nyumba imebomoka walisema hama, kwahiyo nyumba hizi inawezekana zinasikilizwa sana kwa watu wenye hela,” amesema Msamba.

Kaimu Meneja wa TBA, Mkoa wa Dar es Salaam, Bernard Mayemba amekiri kuwepo kwa uchakavu wa majengo hayo huku akisema Moja ya vitu vinavyorudisha nyuma utekelezaji wa ukarabati wa nyumba hizo ni pomoja na kuwepo kwa wapangaji ambao ni wadaiwa sugu, huku wengine wakidiriki kuwauzia watu maeneo yao wajenge nyumba.