May 17, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

DKT.Samia muumini namba moja wa maridhiano nchini-Dkt.Biteko

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko amesema kuwa, Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan amekuwa muumini namba moja wa maridhiano nchini na haishii katika kusema tu bali anatekeleza kwa vitendo huku nia ikiwa ni kuhakikisha kunakuwa na umoja na amani nchini.

Dkt. Biteko amesema hayo Desemba 10 , 2023 wakati wa misa maalum ya kutabaruku Kanisa Kuu la Kiinjili la Kilutheri Tanzania ( KKKT) Lukajange, Dayosisi ya Karagwe iliyofanyika wilayani Karagwe, Mkoa wa Kagera.

Misa hiyo maalum imehudhuriwa na Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi ( CCM), Bara, Komredi Abdulrahman Kinana , Waziri wa Ujenzi,Innocent Bashungwa na Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Fatma Mwasa.

“Rais, Dkt. Samia anasema kila mara kuwa hii nchi ni yetu sote, anatuasa mara nyingi kuwa wewe kama ni CCM mpende mpinzani, na mpinzani mpende CCM, tuungane pamoja tusukume nchi yetu mbele,akaunda Kamati ya Kitaifa ya Maridhiano ambayo imejumuisha makundi mbalimbali wakiwemo wanasiasa kutoka vyama mbalimbali na viongozi wa dini ili kuwe na muafaka nchini, tujenge Tanzania bora kwa ajili yetu na vizazi vijavyo,”amesisitiza Dkt. Biteko.

Ameongeza kuwa, Rais Samia amekuwa muumini wa maridhiano si kwa kuigiza bali kwa dhati ya moyo wake na ameonesha mifano mbalimbali ya maridhiano ikiwemo kuwa mgeni rasmi katika Baraza la Wanawake wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo ( CHADEMA) wilayani Moshi na hicho ni kiashirikia kikubwa cha kuonesha kuwa anataka umoja na amani nchini.

Vilevile, Dkt. Biteko ameendeelea kusisitiza kuwa, Serikali inaunga mkono madhehebu ya dini na shughuli za kidini nchini na ndiyo maana imeendelea kutoa uhuru wa kuabudu kwa kila Mtanzania.

Katika hatua nyingine, Dkt.Biteko ametaka viongozi mbalimbali nchini kufanya kazi  na watu wanaowaunga mkono na wasiowaunga mkono kwani wajibu wao ni kuwahudumia wananchi wote.

Kuhusu utekelezaji wa miradi ya maendeleo amesema kuwa, miradi inaendelea kutekelezwa katika sekta mbalimbali ikiwemo za nishati, miundombinu,afya ili kuelekea katika Tanzania tunayoitaka.

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Bara, Komredi Abdulrahman Kinana amempongeza Askofu Benson Bagonza kwa uongozi mzuri katika Dayosisi ya Karagwe na ujenzi wa Kanisa Kuu jipya katika Dayosisi hiyo.

Pia amewapongeza Mashemasi Watano katika Dayosisi hiyo ambao wamepata Uchungaji.

Waziri wa Ujenzi, ambaye pia ni Mbunge wa Karagwe, Innocent Bashungwa  amepongeza ujenzi wa kanisa hilo kuu na pia amempongeza Askofu Benson Bagonza kwa kufanya kanisa katika Dayosisi hiyo kuzidi kusonga mbele. Pia ameahidi kushirikiana nao katika kujenga Dayosisi hiyo.

Kwa upande wake, Askofu wa Dayosisi ya Karagwe, Benson Bagonza amemshukuru Rais Samia kwa kusimamia  suala la maridhiano kwa makundi yanayoonesha kukinzana huku akisema kuwa upatanisho huo anaousimamia una baraka za Mungu na amemtia moyo wa kuendelea kitasimamia kwani ni afya kwa taifa.

Aidha, amemshukuru Rais, Dkt. Samia, pamoja na  viongozi mbalimbali wa Serikali waliochangia ujenzi wa Kanisa Kuu la KKKT, Dayosisi ya Karagwe pamoja na waumini na wadau mbalimbali.

Pia, Askofu Bagonza ametoa pole kwa Serikali na Wananchi kufuatia vifo na majeruhi vilivyotokana na janga la kiasili wilayani Hanang, mkoani Manyara.

Dayosisi ya Karagwe ilizinduliwa mwaka 1979 ambapo ujenzi wa kanisa hilo kuu ulianza Februari 24, 2023 na kukamilika Novemba 2023 ambao umegharimu milioni 400.