Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online
CHAMA cha Mpira wa Wavu Nchini (TAVA) kinaendelea na maandalizi kuelekea kwenye mafunzo ya ndani ya awali na ya kitaifa (National and Candidate referee course) yatakayoanza rasmi Septemba 28 hadi Oktoba 3 katika viwanja vya JMK Park.
Kozi hiyo iliyoandaliwa na Kamisheni yake ya Waamuzi inalenga kuimarisha fani ya uamuzi kwa waamuzi wapya na wale ambao walipata kozi ya awali (Candidate referees) mwaka 2017, na waamuzi wa kitaifa (National referees).
Katibu Mkuu wa chama hicho, Alfred Selengia ameliambia Majira kuwa, hadi sasa zaidi ya wadau 45 wameonesha nia ya kushiriki kozi hiyo ambayo yatagusa makundi matatu.
Kiongozi huyo ambaye pia ni mkufunzi wa kwanza wa makocha wa mpira wa Wavu na Wavu Ufukweni kutoka Tanzania na Afrika kwa ujumla amesema, kundi la kwanza ni wale watakaoshiriki kozi ya awali (walimu shile za msingi na Sekondari) kwani michjezo mingi ya UMISETA na IMITASHUMTA wamekuwa wakiisimamia wenyewe hivyo mafunzo hayo yatasaidia kujua sheria, kanuni na taratibu zinazoongoa mchezo huo.
Selengia amesema kuwa, kundi la pili ni watakaoshiriki kozi ya ngazi ya kitaifa (National Referees) ambayo itahusishwa wale walioshiriki kozi ya awali (Candidate referees) mwaka 2017 huku kundi la tatu ni kwa wale watakaoshiriki kozi ya ‘reflesher course’.
“Hadi sasa tayari zaidi ya wadau 45 wameonesha nia ya kutaka kushiriki hivyo na sisi tunaendelea na maandalizi kwani kwa wale walioshiriki kozi ya ngazi ya kitaifa (National referees) watashiriki ‘reflesher’ ambapo watajadili sheria na mifumo mipya ya uchezeshaji, ” amesema Selengia.
Hivi karibuni Katibu hiyo aliuambia mtandao huu kuwa, atahakikisha anazalisha wakufunzi wengi zaidi wa mchezo huo ambao wataweza kutoa elimu kwa walimu wa Shule za msingi na sekondari Tanzania nzima ili kuibua vipaji vya watoto.
Lakini pia wanataka waweze kutumika katika mashindano mbalimbali kuanzia yale ya Umitashumta na Ummiseta ambayo yamekuwa yakizalisha wachezaji wazuri wanaochipukia.
“Baada ya kuteuliwa na Shirikisho la Mpira wa Wavu Afrika (CAVB) kuwa mkufunzi wa kwanza wa makocha wa mpira wa wavu kutoka Tanznaia na Afrika kwa ujumla, moja ya mikakati yangu ilikuwa kuzalisha wakufunzi wengi ambao nao wataweza kutoa mafunzo kwa walimu mbalimbali lengo likiwa ni kukuza na kuupa thamani kubwa mchezo huu hapa nchini,” amesema Selengia.
Baada ya kupata wakufunzi hao kuna uwezekano mkubwa wa kuzalisha wachezaji bora watakaoweza kuwa msaada mkubwa kwa kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania ambayo itakuwa na maboresho makubwa katika siku zijazo.
Lakini pia mikakati mingine aliyopanga kutekeleza ni kuongeza idadi ya wachezaji wa timu hiyo ambao ushindani watakaouonesha ndio utakaowapa nafasi ya kuwakilisha nchi katika mashindano ya kimataifa.
Itakumbukwa kuwa, tayari Selengia ameshaanza kutekeleza mpango huo kwa kuisaidia timu hiyo kutinga hadi hatua ya pili katika mashindano ya hatua ya pili ya Kanda ya Tano ya Afrika ya Wavu Ufukweni ya kuwania kufuzu kushiriki mashindano ya Olimpiki ‘Africa sub Zonal V Olympic qualifiers 2020’ yaliyokuwa yaanze kutimua vumbi kati ya Machi 16, 2020 na Aprili 30, 2020 kabla ya kuahirishwa kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa Corona.
Tanzania ilifanikiwa kutinga katika hatua hiyo ya pili baada ya kufanikiwa kufanya vizuri katika mashindano ya awali yaliyofanyika katika fukwe za Lido zilizopo Entebbe, Uganda ambapo ilifanikiwa kushinda mechi zake zote dhidi ya Uganda, Kenya na Sudan na kufanikiwa kukaa juu ya msimamo wa kundi lao wakifuatiwa na Kenya ambao nao walifuzu kutinga hatua ya pili huku Sudan wakishika nafasi ya tatu na Uganda wakikaa nafasi ya mwisho.
Katika hatua hiyo, Tanzania alichaguliwa kuwa mwenyeji wa mechi za Kundi B pamoja na timu za Taifa za Ghana, Afrika Kusini, Sudan na Niger ambapo mashindano hayo yalipangwa kufanyika kati ya Machi 26 hadi 30.
Alisema, mikakati iliyopo sasa ni kuhakikisha Tanzania inaweka rekodi kubwa kwa kufika mbali katika mashindano hayo na mengine ya kimataifa ya mchezo huo na watahakikisha wanafanya kila liwezekanalo kuifanikisha kwa wakati.
More Stories
Watumishi wa Fahari wafanya Bonanza
Rais Samia atia mkono mchezo wa masumbwi Tanzania
Chino bingwa mpya wa IBA Intercontinental Championship